Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya nusu ya watu wote duniani wanakosa huduma ya afya-ILO

Mtoto mwenye umri wa miaka 9 akipata chanjo. Katika maeneo mengine duniani, upatikanaji wa huduma za afya kama hizi zimekuwa ni changamoto.
UNICEF/UN0253234/Moreno Gonza
Mtoto mwenye umri wa miaka 9 akipata chanjo. Katika maeneo mengine duniani, upatikanaji wa huduma za afya kama hizi zimekuwa ni changamoto.

Zaidi ya nusu ya watu wote duniani wanakosa huduma ya afya-ILO

Afya

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la kazi ulimwenguni iliyotolewa hii leo mjini Geneva Uswisi, zaidi ya nusu ya idadi ya watu wote duniani wanakosa huduma ya afya na ni asilimia 29 tu ambao wanapata huduma kwa mfumo wa bima ya afya.

Ripoti hiyo kuhusu ulinzi wa jamii katika nchi 100 imeeleza kuwa, kidunia, ni asilimia 68 tu ya watu wa umri wa kustaafu ambao wanapokea namna fulani ya kiinua mgongo, na kuwa katika nchi nyingi za kipato cha chini, asilimia hizi zinashuka zaidi kufikia asilimia 20. Nchi chache kufikia asilimia 60 ziliripoti kuwa na mfumo au mafao ya kuhakikisha uhakika wa kipato kwa watoto.

Matokeo haya ni ya utafiti uliokusanywa na kamati ya wataalamu wa ILO ikijikita katika mapendekezo ya ILO kuhusu ulinzi wa jamii ambayo inatoa wito kuwa na uhakika wa kipato na huduma za kiafya kuanzi katika utoto hadi utu uzima. Pia inahamasisha kuwa na ulinzi kwa watu wengi zaidi iwezekanavyo na pamema iwezekanavyo.

Emmanuelle St-Pierre Guilbault, mtaalamu wa sheria wa ILO katika idara ya viwango vya kimataifa vya kazi anasema, “ILO iko tayari kuzisaidia nchi kushughulikia vikwazo vilivyosalia ikiwemo masuala mazito ya kifedha, katika kuelekea ulinzi wa jamii wa uhakika kwa wote.”

Utafiti huo unasema japokuwa huduma ya kiafya imefikiwa katika nchi nyingi za kipato cha juu na cha kati, lakini katika nchi nyingi, watu wengi wanapata aina fulani Fulani tu za huduma za afya.

Upungufu uliotajwa ni pamoja na fedha kidogo zinazoelekezwa katika afya na upungufu wa wataalamu wa afya hali ambayo inatokana na ugumu wa uchumi ambao ulionekana katika maeneo yote duniani.

Ripoti inasema juhudi zinahitajika kuanzisha mfumo wa bima ya afya kwa wote kisheria na kwa vitendo ikiwemo kupanga upya bajeti na kuelekeza fedha katika sekta ya afya na vilevile kuongeza idadi ya wafanyakazi wa afya.

Ulinzi wa jamii linategemewa kuwa katika agenda za mkutano mkuu wa ILO mwaka 2020.