Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kituo kipya kusaidia wakimbizi wa Venezuela chafunguliwa:UNHCR

Wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela wakijipanga kupokea chakula kinachosambwaza na UNHCR. Inakadiriwa kila siku UNCHR inalazimika kuwapatia chakula watu 5,000 katika mpaka wa Colombia na Venezuela.
UNHCR/Siegfried Modola
Wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela wakijipanga kupokea chakula kinachosambwaza na UNHCR. Inakadiriwa kila siku UNCHR inalazimika kuwapatia chakula watu 5,000 katika mpaka wa Colombia na Venezuela.

Kituo kipya kusaidia wakimbizi wa Venezuela chafunguliwa:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Kituo kipya kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wasiojiweza na walio hatarini kutoka Venezuela kimefunguliwa leo kwa ushirikiano wa serikali ya Colombia na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Kituo hicho kitakachojikita katika kutoa msaada kitakuwa kwenye mpaka baina ya Venezuela na Colombia kwenye mji wa Maicao jimbo la Laguajira.

Kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR mjini Geneva Andreh Mahecic kituo hicho cha msaada kimewekwa kwa ombi la viongozi wa kitaifa na kijamii na kina uwezo wa awali wa kuhifadhi watu 30 lakini kuna uwezekano wa kukipanua ili kiweze kuhifadhi watu wengi zaidi katika siku za usoni.

Ameongeza kuwa watu wasiojiweza kutoka Venezuela watapata fursa ya muda ya malazi, chakula, maji, huduma za msingi za afya na huduma nyingine katika kituo hicho.

Kituo hicho ambacho ni cha kwanza cha aina yake nchini Colombia kinalenga kushughulikia kwa muda mahitaji ya dharura ya kibinadamu na mahitaji ya ulinzi kwa watu wanaokimbia kutoka Venezuela na kupia kusaidia uongozi wa jamii ya eneo hilo kukabiliana na wimbi kubwa na wakimbizi na wahamiaji.

Maicao ni moja yay a miji ya jimbo la La Guajira iliyo na msongamano mkubwa wa wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela.

Mamia ya watu wakiwemo Watoto, wazee, watu wenye ulemavu na wagonjwa mahtuti wanalazimika kuishi mitaani kutokana na kutokuwepo kwa malazi mbadala.

Kwa mujibu wa tathimini ya karibuni ya UNHCR idadi kubwa ya Wavenezuela mjini Maicao wanaishi mitaani au katika makazi yasiyo rasmi na asilimia 81 ya waliohojiwa wamesema wanahitaji malazi.Zaidi ya Wavenezuala milioni 3.4 wanishi nje ya nchi na milioni 2.7 lati yao waliondoka nchini mwao tangu mwaka 2015.

Na ili kusaidia juhudi za serikali ya Venezuela kutoa ulinzi wa kimataifa na kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu ya raia wa Venezuela wanaowasili UNHCR inafanya juhudi kuimarisha mitandao ya malazi, kutoa msaada wa kisheria na kuwezesha fursa ya kupata chakula , maji, elimu na huduma za afya.

Mwaka huu wa 2019 UNHCR inahitaji dola milioni 78 ili kukidhi mahitaji ya Wavenezuela 500,000 na jamii zinazowahifadhi katika nchi 16 duniani.