Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto waliozaliwa na wazazi wa Venezula nchini Colombia sasa kupewa uraia:IOM

Tarehe 24 Aprili 2019 mjini Cucuta Colombia mtoto akimkumbatia mama yake katika kituo cha wasamaria wema cha kupumzikia kwa watu wanaotembea ambao wataendelea na safari yao ya mguu kutoka Venezuela wakilenga kuingia Cali Colombia
UNICEF/Arcos

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM leo limekaribisha uamuzi uliofanywa na serikali ya Colombia wa kuwapa uraia watoto waliozaliwa nchini humo kutokana na wazazi ambao ni raia wa Venezuela. 

Kwa mujibu wa IOM hatua hiyo itawafaidisha Watoto Zaidi ya 24,000 ambao wako katika hatari ya kutokuwa na utaifa.Shirika hilo linasema hatua hii muhimu na za muda ambazo zilitangazwa jana Jumatatu Agosti 5 na Rais wa Colombia Iván Duque, zinathibitisha ahadi ya serikali ya nchi hiyo katika utekelezaji wa haki za binadamu na mikataba ya kimataifa kwa kuwahakikishia wasichana na wavulana haki ya kuwa na utaifa bila kujali hadhi yao ya uhamiaji.

“Azimio hili ni mchango mkubwa katika kuelekea uhamiaji salama na wa kawaida ambao hatimaye utawezesha kutambuliwa kwa haki ya msingi ya Watoto wa Venezuela pamoja na kuchangia kujumuishwa kwao katika jamii” amesema Ana Durán Salvatierra, mkuu wa ofisi ya IOM nchini Colombia.

Azimio hilo jipya la serikali ya Colombia litaanza kutekelezwa rasmi 20 Agosti 2019 na litawajumuisha watoto waliozaliwa nchini Colombia tangu 19 Agosti 2015. Kwa hatua hiyo IOM inasema serikali ya Colombia itasaidia kuzuia Watoto hawa wasiojiweza kuwa watu wasio na utaifa n ani hatua muhimu kuelekea hakikisho la ulinzi wao.

Wakimbizi kutoka Venezuela waliokimbilia Colombia, Takriban watu 5,000 wamekuwa wakivuka mpaka kuondoka Venezuela kila siku kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Aprili 2019.
©UNHCR/Vincent Tremeau
Wakimbizi kutoka Venezuela waliokimbilia Colombia, Takriban watu 5,000 wamekuwa wakivuka mpaka kuondoka Venezuela kila siku kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Aprili 2019.

IOM kwa kushirikiana na kitengo cha idadi ya watu, wakimbizi na wahamiaji cha idara ya mambo ya ndani ya Marekani (PRM) wataisaidia kiufundi ofisi ya usajili ya Colombia katika utekelezaji wa azimio hili pamoja na kusambaza kampeni ya Primero la Niñez.

Kampeni hiyo inalenga kuwataarifu watu husika jinsi gani ya kufikia hatua hiyo, muongozo wa kufuata, hatua za kuchukua, tarehe azimio litakapoanza kutekelezwa na wajibu wa kila kitengo.

Kwa mujibu wa idara ya uhamiaji ya Colombia hadi kufikia 30 Juni 2019 kulikuwa na raia zaidi ya milioni 1.4 wa Venezuela nchini Colombia ambayo ni nchi ya kwanza kupokea wakimbizi katika kanda hiyo.

Katika juhudi zake za kuisaidia serikali katika kampeni hii IOM inaungana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuhudumia wakimbizi UNHCR na la kuhudumia watoto UNICEF.