Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baba alipofariki dunia ndipo FGM ikawa tishio kwetu, Masanga iliniokoa- Msichana Elizabeth

Visu vya mangariba sasa vitasalia butu kwa kuwa watoto wa kike, wanawake na jamii zimefunguka macho juu ya madhara ya ukeketeaji au FGM.
UNICEF/Holt
Visu vya mangariba sasa vitasalia butu kwa kuwa watoto wa kike, wanawake na jamii zimefunguka macho juu ya madhara ya ukeketeaji au FGM.

Baba alipofariki dunia ndipo FGM ikawa tishio kwetu, Masanga iliniokoa- Msichana Elizabeth

Afya

Kuelekea siku ya kimataifa hapo kesho ya kutokomeza ukeketaji wa watoto wa kike na wasichana duniani, FGM, nchini Tanzania, kituo ambacho ni kimbilio kwa watoto wanaokwepa mila hiyo potofu, kimeendelea kuwaepusha watoto wa kike na wao sasa ni mashuhuda. 

Kituo hicho cha Masanga, kilichopo mkoani Tarime mkoani Mara kinatoa mafunzo ya ukeketaji mbadala na tohara salama na ni kimbilio la watoto wanaokwepa mila hiyo.

Mmoja wa wanufaika ni Elizabeth Magabe ambaye katika mahojiano na Bright Warren wa shirika la idadi ya watu duniani, UNFPA, wafadhili wa kituo  hicho anasema alijiunga na kituo mwaka 2012 lakini, "nilikuwa naishi na wazazi wangu wote, lakini baba yangu kufariki duniani, ambaye alikuwa ndiye mtetezi wetu dhidi ya ukeketaji, hapo  ndipo tukaanza kupata changamoto. Ilipofikia mwaka 2014 wakati ukeketaji ndio umepamba moto, ndipo dada yangu mmoja akawa anatoka shule alipofika nyumbani likizo, wakamlazimisha na kumkeketa."

Uwepo wake kwenye kituo ulimnusuru na FGM na ameweza kuhitimu kidato cha nne na sasa ana  ushauri akisema "mimi kwa sasa najiona kwenye familia yangu na kwenye jamii naonekana mwenye thamani na mimi mwenyewe ninajikubali kuwa nina thamani na ninaweza kukubalika kwa kila mtu. Pia nawashauri hata vijana kuwa mtoto wa kisasa ambaye hajakeketwa ni mtoto ambaye anaweza kuleta maendeleo makubwa sana katika jamii. Hata ukiangalia katika jamii yetu ya kikuria, wasichana ambao wamekeketwa hawaleti maendeleo yoyote yale.  Lakini kwa upande wangu wasichana ambao hatujakeketwa tuko tayari kuleta maendeleo na kufanya kitu kikubwa katika jamii  yetu."

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinasema kuwa hivi sasa kuna wanawake na wasichana zaidi ya milioni 200 ulimwenguni kote ambao wamekeketwa.