Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jedwali la elementi latimiza miaka 150, UN yapongeza maadhimisho hayo

Wanafunzi wakiangalia jedwali la elementi au Periodic Table katika shule ya wasichana huko Herat, Afghanistan.
Graham Crouch/World Bank
Wanafunzi wakiangalia jedwali la elementi au Periodic Table katika shule ya wasichana huko Herat, Afghanistan.

Jedwali la elementi latimiza miaka 150, UN yapongeza maadhimisho hayo

Utamaduni na Elimu

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO,  leo limezindua mwaka wa kimataifa wa jedwali la elementi kwa kiingereza Periodic Table katika makao yake makuu mjini Paris Ufaransa, ukiwa ni mwanzo wa mfululizo wa matukio na shughuli mbalimbali zitakazofanyika kwa mwaka mzima, wakati dunia ikiadhimisha miaka 150 tangu kuundwa kwa jedwali hilo na mwanasaynsi wa Urusi Dimtri Mendeleev.

Uamuzi uliofanywa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa miaka miwili iliyopita wa kuufanya mwaka huu 2019  kuwa wa maadhimisho ya kemia unalenga kutambua umuhimu wa jedwali hilo lenye orodha ya elementi kwa kuzingatia uzito wake wa atomu kama “moja ya mafanikio muhimu na yenye ushawishi katika ulimwengu wa sayansi, ikimulika chimbuko sio tu la kemia, bali pia fizikia, baolojia na masomo mengine ya sayansi.”

Uzinduzi huo wa leo mjini Paris umewaleta pamoja wanasayansi na wawakilishi wa sekta binafsi na umefanywa na mkurugenzi mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay, mbele ya wageni wengine mashuhuri kama Mikhail Kotyukov ambaye ni waziri wa sayansi na elimu ya juu wa Urusi, Pierre Corvol , Rais wa jumuiya ya elimu ya sayansi wa Ufaransa na profesa Ben Feringa mshindi wa mwaka 2016 wa tuzo ya amani ya Nobel upande wa Kemia.

Katika maadhimisho ya mwaka mzima, UNESCO itawasilisha mradi wake wa elimu ujulikanao kama “uvumbuzi 1001:safari kutoka ukemia hadi kemia” wenye lengo la kuwasaidia vijana katika mashule kote duniani kuimarisha uelewa wao wa masuala ya kemia na matumizi yake.

Matukio mengine yatakayofanyika kuambatana na maadhimisho ya mwaka huu ni pamoja na mijadala iliyopangwa kufanyika mjini Paris Ufaransa na Murcia Hispania, lakini pia shindalo litakalofendeshwa mtandaoni kupima ufahamu na kuzusha udadisi wa wanafunzi wa sekondari kuhusu somo la kemia.