Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi yasababisha ukosefu wa amani na usalama.

Huko Puntland, Somalia, mimea inakauka, mifugo inakufa kutokana na ukame kwenye eneo hilo, kufuatia mfululizo wa miaka mitatu ya ukosefu wa mvua (Picha ya mwaka 2017).
UNDP Somalia/Said Isse
Huko Puntland, Somalia, mimea inakauka, mifugo inakufa kutokana na ukame kwenye eneo hilo, kufuatia mfululizo wa miaka mitatu ya ukosefu wa mvua (Picha ya mwaka 2017).

Mabadiliko ya tabianchi yasababisha ukosefu wa amani na usalama.

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wa wazi kuangazia jinsi gani mabadiliko ya tabianchi yanasababisha ukosefu wa amani na usalama duniani, mkutano uliongozwa na waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Dominica Miguel Vargas.

Akihutubia mkutano huo, Mkuu wa idara ya siasa katika Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo amesema madhara hayo ni hatari kwa dunia nzima lakini yamekuwa yakihisiwa zaidi na maeneo ambayo tayari yako hatarini.

Di Carlo ameliambia baraza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaathiri amani na usalama si moja kwa moja lakini katika hali mbaya zaidi.

Mathalani katika eneo la Sahel mapambano ya kugombea rasilimali kati ya wakulima na wafugaji katika bonde la ziwa Chad yamepunguza fursa za kiuchumi na kutishia maisha ya watu “katika siku za hivi karibuni, baraza limetambua matokeo ya mabadiliko ya tabianchi miongoni mwa sababu nyingine kwenye ukosefu wa amani nchini Mali, Somalia, Afrika Magharibi na Sahel, Afrika ya kati na Sudan”

Rosemary A. DiCarlo, Mkuu wa masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama
UN/Eskinder Debebe
Rosemary A. DiCarlo, Mkuu wa masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama

Wajumbe wa baraza pia wamemsikiliza mwanasayansi mkuu wa shirika la dunia la hali ya hewa WMO bwana Pavel Kabat ambaye amesema, “mabadiliko ya tabianchi yana madhara makubwa katika usalama, yanarudisha nyuma ongezeko la lishe na upatikanaji wa chakula, husababisha moto wa nyika na pia migogoro ya maji inayosababisha kuongezeka kwa wakimbizi wa ndani na wahamiaji”

Naye Katibu Mkuu wa wizara ya mambo ya nje ya Maldives, Abdulla Shahid katika hotuba yake kwa baraza amesema, “mabadiliko ya tabianchi kwa miaka mingi yanaharibu nchi yetu ambayo ni kisiwa kidogo. Yanamomonyoa fukwe zetu, yanaua matumbawe ambayo yanavilinda visiwa vyetu, yanachafua maji yetu kwa kuyachanganya na maji ya bahari na idadi ya samaki wetu inapungua. Lakini muhimu zaidi mabadiliko ya tabia nchi yatatunyang’anya makazi yetu.”

Mabadiliko ya tabianchi kwa muda mrefu yanachukuliwa kama tishio kwa visiwa kama Maldives ambavyo ardhi yake iko karibu sana na usawa wa bahari.