Kuongezeka kwa ukatili Gaza kunatishia kuzuka kwa vita- DiCarlo

22 Agosti 2018

Mkuu wa masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kuwa kuongezeka kwa ghasia kunatishia vita Gaza na kwamba msaada wa kibinadamu kwa ajili ya ukanda huo haupaswi kuzuiliwa kwa kuangalia mabadiliko ya kisiasa na kiusalama.

Akihutubia Baraza la Usalama Jumatano leo Bi. DiCarlo amesema hali ya kibinadamu Gaza inaendelea kudorora katika wiki chache zilizopita kwa sababu ya vikwazo vinavyowekwa na Israeli juu ya bidhaa zinazoingia kwenye ukanda huo kupitia Kerem Shalom kufuatia kitendo cha wapalestina kurusha vishada na maputo kuelekea Israel.

Amesema tangu ripoti yake ya mwisho kwa baraza hilo tarehe 28 mwezi Juni mwaka huu, Palestina imelenga Israeli kwa kurusha makombora 195 na huku Israeli nayo ikilenga maeneo ya Gaza takriban mara 125.

Kufuatia hali hiyo waPalestina 8 waliuawa ikiwemo mwanamke mjamzito na mwanae mwenye umri wa miezi 18. Wakati huo huo waPalestina wengine 56 na waIsraeli 28 walijeruhiwa. Amesema matukio hayo ni ishara ya udhaifu wa vipindi vya muda vya mfupi vya amani  na umuhimu wa suluhu ya muda mrefu.

 

Rosemary DiCarlo, Mkuu wa masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa, akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Mashariki ya Kati
UN /Loey Felipe
Rosemary DiCarlo, Mkuu wa masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa, akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Mashariki ya Kati

Bi. DiCarlo ameongeza kuwa Katibu Mkuu amekaribisha uamuzi wa kufungua mpaka wa kuvuka Agosti 15 lakini kuongeza kuwa anafuatilia kufungwa kwa eneo la kutembea kwa raia Agosti 19 na Israeli kuzuia wakazi wa Gaza na ukingo wa magharibi wa mto Jordan isipokuwa kwa ajili ya misaada ya kibinadamu.

Bi DiCarlo akikumbusha azimio la Baraza la Usalama la kuondoa vizuizi hivyo amesema, “wakati tukifanya kazi kuondoa kabisa vikwazo dhidi ya Gaza kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama 1860, natoa wito kwa pande zote kuhakikisha kwamba misaada kwa ajili ya mahitaji ya dharura inafikia ukanda. Misaada haipaswi kushikiliwa kwa kuzingatia mabadiliko ya kisiasa na kiusalama. Aidha ninarejelea wito wa awali na mratibu maalum kwa ajili ya Hamas kutoa tarifa kamili kuhusu raia wa Israeli wanaoshikiliwa Gaza kwa mujibu wa sheria za kimataifa.”

 

Ghasia huko Gaza zilianza tarehe 30 mwezi Machi mwaka huu na mtoto huyu ni miongoni mwa majeruhi wa ghasia hizo.
Save the Children/Mohamed N Ali
Ghasia huko Gaza zilianza tarehe 30 mwezi Machi mwaka huu na mtoto huyu ni miongoni mwa majeruhi wa ghasia hizo.

Ameongeza kuwa wpPalestina 13 waliuawa wakati wa maandamano katika uzio wa Gaza, ikiwemo mhudumu mmoja wa afya na watoto wanne huku wapalestina elfu moja na askari jeshi mmoja wa Israeli wakijeruhiwa. Kwa mantiki hiyo ameongeza, “wakati Israeli ina wajibu wa kulinda raia wake, ni lazima ijizuie katika matumizi ya risasi na ijizuie kutumia nguvu kupita kiasi ispokuwa kama hatua ya mwisho. Aidha ametolea wito Hamas kuepukana na ukatili katika ua na kutowaweka watoto katika hatari akiongeza kuwa watoto hawapswi kulengwa au kutumikishwa kwa njia yoyote.”

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter