Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulio yakwamisha uwasilishaji wa misaada muhimu Borno, Nigeria-OCHA

Mtazamo wa mji wa Rann, jimbo la Borno, Kasakzini-Mashariki mwa Nigeria. Julai 5, 2018
WFP/Inger Marie Vennize
Mtazamo wa mji wa Rann, jimbo la Borno, Kasakzini-Mashariki mwa Nigeria. Julai 5, 2018

Mashambulio yakwamisha uwasilishaji wa misaada muhimu Borno, Nigeria-OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Nigeria, Edward Kallon ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuzuiwa kwa uwasilishaji wa misaada kwa makumi ya maelfu ya wakimbizi wa ndani walioko mjini Rann, mashariki mwa jimbo la Borno, karibu kilometa kumi mpakani na Cameroon kufuatia shambulio la kundi lililojihami.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu ya Umoja nwa Mataifa, OCHA, imesema usitishwaji huo wa misaada huko Rann unatokana na shambulio lililoanza jioni ya tarehe 14  mwezi huu wa Januari katika kituo cha jeshi na kuendelea hadi siku iliyofuatia ambapo wakati wa shambulio hilo inakadiriwa kuwa watu 76,000 wakimbizi wa ndani walikuwa wanaishi mji huo.

Kituo cha afya, maghala yaliyokuwa yamehifadhi misaada ya kibinadamu na makazi ya watoa huduma yaliporwa na kuharibiwa wakati wa shambulio hilo huku soko na makazi kambini yaliteketezwa. 

Kufuatia tukio hilo watoa huduma 14 waliokuwa katika mji wa Rann wakati wa shambulio hilo wamesafirishwa kwa njia ya helikopt na sasa mji wa Rann hakufikiki kwa njia ya barabara au anga.

Akizungumzia shambulio hilo Bwana Kallon amesema, “mashambulizi mjini Rann yanaongezeka na kuathiri vibaya raia wanaosaka hifadhi katika mji huo uliojitenga na kuathiria uwasilishaji wa misaada kwa wanawake, wanaume na watoto walio na mahitaji.”  Ameongeza kuwa, “shambulio hilo limesababisha hofu kwa watu ambao tayari walikuwa hatarini”.

Kwa mantiki hiyo Bwana Kallon ametoa wito kwa serikali ya Nigeria kulinda raia ikiwemo wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu.

Mzozo katika maeneo ya kaskazini-mashariki mwa Nigeria, sasa katika mwaka wake wa 10 umesababisha watu wengi kufurushwa na janga kubwa la kibinadamu ambapo takriban watu milioni saba wanamahitaji. 

Isitoshe shambulio la Rann na  uhasama katika maeneo ya Kukawa na Monguno kaskazini mwa jimbo la Borno limesababisha zaidi ya watu 43,000 kukimbia makwao tangu Novemba mwaka jana, huku zaidi ya watu 32,000 wakisaka hifadhi Maiduguri mji mkuu wa Borno.