Watoto zaidi ya 3,500 wametumiwa na makundi yenye silaha Nigeria tangu 2013:UNICEF

12 Aprili 2019

Katika kuaelekea maadhimisho ya miaka mitano tangu kutekwa kwa watoto wa Chibok nchini Nigeria, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limetaka kuwepo kwa ulinzi zaidi wa haki za watoto. 

Kwa mujibu wa taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo zaidi ya watoto 3,500 wengi wakiwa na umri wa kati ya miaka 13 hadi 17 waliingizwa na kutumiwa katika vita vinavyoendelea Kaskazini Mashariki mwa Nigeria na makundi yenye silaha yasiyo ya kiserikali .

Shirika hilo limesema na idadi hii ni wale tu ambao wamethibitishwa lakini idadi kamili inaweza kuwa kubwa zaidi. Mbali ya idadi hiyo watoto wengine 432 wameuawa au kujeruhiwa, 180 kutekwa nyara na wasichana 43 kutendewa ukatili wa kingono Kaskazini Mashariki mwa Nigeria mwaka 2018.

Wakati huohuo shirika hilo linasema zaidi ya wasichana 100 wa Chibok waliotekwa nyara bado hawajapatikana hadi leo. Maadhimisho ya kutekwa kwa wasicha wa Chibok hufanyika kila Aprili 14 na kwa mujibu wa UNICEF ni kumbusho kwamba utekaji wa watoto na ukiukwaji mkubwa wa haki zao unaendelea Nigeria.

UNHCR/George Osodi
Mtoto wa miaka 8 akiwa ameketi kibarazani mkiwa bila wazazi wala walezi kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Fufore jimboni Adamawa , Kaskazini Mashariki mwa Nigeria

Mwakilishi wa UNICEF nchini Nigeria Mohamed Malick amesema “Watoto wanastahili kujihisi wako salama nyumbani, mashuleni na kwenye viwanja vya michezo wakati wote . Tunatoa wito kwa pande zote katika mzozo kutimiza wajibu wao chini ya sheria za kimataifa na kukomesha ukiukwaji wa haki dhidi ya watoto na kuacha kuwalenga raia na miundombinu yao zikiwemo shule. Hii ni njia pekee itakayotufanya tuanze kupiga hatua za kuboresha maisha ya watoto katika eneo hili la Nigeria lililoathirika na vita.”

Tangu mwaka 2012 makundi yenye silaha yasisyo ya kiserikali Kaskazini Mashariki mwa Nigeria yamewaingiza na kuwatumia watoto kama wapiganaji  na sio wapiganaji vitani, yamewabaka na kuwashurutisha wasicha kuolewa nao, na pia yametekeleza ukiukwaji mkubwa mwingine wa haki dhidi ya watoto. Baadhi ya wasicha hao wamepata ujauzito wakiwa matekani na kujifungua bila hata huduma za kitabibu.

UNICEF inasema inaendelea kutoa msaada kwa serikali ya Nigeria katika juhudi zake za kuwalinda watoto wa taifa hilo. Na inashirikiana na wizara ya masuala ya wanawake na maendeleo ya jamii ya jimbo la Borno na wadau wengine, ili kuwasaidia watoto ambao wameokolewa au wametoroka kutoka walikokuwa wakishikiliwa mateka.

Mwaka 2017 na 2018 UNICEF na washirika wake walifanikiwa kutoa huduma ya kuwajumuisha tena katika jamii zaidi ya watu 9,800 wakiwemo watoto ambao walikuwa wakijihusisha na makundi yenye silaha awali. Na huduma hizo zilisaidia kuzitafuta na kuzibaini familia za watoto hao na kuwarejesha katika jamii zao huku wakipatiwa msaada wa kisaikolojia, elimu, mafunzo ya ufundi, uanagenzi na fursa za kuboresha maisha yao.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter