Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa jina kati ya Ugiriki na Macedonia iliyokuwa Jamhuri ya Yugoslavia unaelekea kupata suluhu: UN

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa jina katika ya Ugiriki na Macedonia iliyokuwa Jamhuri ya Yugoslavia (FYROM), Matthew Nimetz.
UN Photo/Rick Bajornas)
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa jina katika ya Ugiriki na Macedonia iliyokuwa Jamhuri ya Yugoslavia (FYROM), Matthew Nimetz.

Mgogoro wa jina kati ya Ugiriki na Macedonia iliyokuwa Jamhuri ya Yugoslavia unaelekea kupata suluhu: UN

Amani na Usalama

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa jina katika ya Ugiriki na Macedonia iliyokuwa Jamhuri ya Yugoslavia (FYROM), Matthew Nimetz, amepokea uamuzi wa bunge la Jamhuri hiyo ya zamani ya Yugoslavia wa kupitisha makubaliano kuhusu jina jipya la nchi hiyo kufuatia mgogoro ambao umedumu kwa miaka 28.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Bwana Nimetz alilipongeza bunge na wananchi wa Macedonia iliyokuwa Jamhuri ya Yugoslavia ambao walipitisha mabadiliko ya jina kupitia kura ya maoni iliyofanyika mwezi Septemba 2018 kwa njia ya kidemokrasia.

Bwana Nimetz kupitia taarifa yake amesema, “makubaliano haya ya kihistoria kati ya majirani hawa yanafungua mlango katika uhusiano mpya kati yao. Ninatizamia kukamilika kwa mchakato kama ulivyoainishwa katika mkataba. Umoja wa Mataifa bado unaendelea kuhakikisha unafanya kazi na pande zote mbili ili hatimaye suluhu ipatikane na tofauti ziishe kati yao”

Hata hivyo kwa nchi hiyo kuweza kubadilishwa jina na kuitwa Jamhuri ya Macedonia ya Kaskazini, lazima Bunge la Ugiriki lipige kura kuidhinisha mpango huo. Jumapili hii imeripotiwa kuwa suala hili limeiingiza serikali ya Ugiriki kwenye mgogoro. Serikali ya umoja wa kitaifa imejikuta ikigawanyika kuhusu mabadiliko ya jina ambapo Waziri Mkuu Alexis Tsipras inaripotiwa kuwa anapanga kuitisha kura ya imani ambayo inatarajiwa kufanyika jumatano ya wiki hii.

Historia ya mgogoro huu wa jina inarejea nyuma hadi mwaka 1991 wakati ambapo Macedonia iliyokuwa Jamhuri ya Yugoslavia FYROM) ilipojitangazia uhuru kwa kujitenga na nchi ya Yogoslavia na wakajitangazia kwamba nchi yao ingeitwa “Macedonia”.

Nchi jirani ya Ugiriki ilikataa kulitambua jina hilo ikisisitiza kuwa ni eneo la kaskazini mwa Ugiriki tu ambalo linaitwa Macedonia linalotakiwa kutumia jina hilo na wakadai kwa FYROM kutaka kulitumia jina hilo ilikuwa ni changamoto kwa himaya ya Ugiriki.