Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wazipongeza Ugiriki na Macedonia kumaliza mgogoro wa tangu mwaka 1991.

Bendera za mataifa mbalimbali katika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi.
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Bendera za mataifa mbalimbali katika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi.

Umoja wa Mataifa wazipongeza Ugiriki na Macedonia kumaliza mgogoro wa tangu mwaka 1991.

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepokea taarifa rasmi ya utekelezaji wa makubaliano ya Prespa ambayo yanafanya kufikiwa muafaka wa kuanza kutumika kwa jina la Jamhuri ya Marcedonia Kaskazini, taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu imeeleza.

Bwana Antonio Guterres ameyapokea makubaliano hayo ambayo yameanza kufanya kazi tangu Februari 12, 2019  na yanayomaliza mgogoro huo wenye historia inayorejea nyuma hadi mwaka 1991 wakati ambapo Macedonia iliyokuwa Jamhuri ya Yugoslavia ya zamani (FYROM) ilipojitangazia uhuru kwa kujitenga na nchi ya Yogoslavia na wakajitangazia kwamba nchi yao ingeitwa “Macedonia.”

Nchi jirani ya Ugiriki ilikataa kulitambua jina hilo ikisisitiza kuwa ni eneo la kaskazini mwa Ugiriki tu ambalo linaitwa Macedonia linalotakiwa kutumia jina hilo na wakadai kwa FYROM kutaka kulitumia jina hilo ilikuwa ni changamoto kwa himaya ya Ugiriki.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezipongeza nchi hizo mbili na mawaziri  wake Alexis Tsipras na Zoran Zaev katika juhudi za kufikia hatua hiyo yenye matazamio ya kuanzisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili zilizokuwa zikivutana.

Aidha bwana Guterres amemshukuru mjumbe wake maalumu Matthew Nimetz kwa kujitolea kwake pasi na kuchoka kufanikisha maafikiano hayo.

Guterres ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, jumuiya za kikanda na washirika wote wa kimataifa kuunga mkono hatua hii ya kihistoria iliyofikiwa na pande zilizokinzana kwa Zaidi ya miaka 20.