Guterres akataa katakata serikali ya Guatemala kusitisha shughuli za CICIG
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Guatemala Sandra Jovel ambapo waziri huyo amemkabidhi Katibu Mkuu barua ya kumwarifu dhamira ya serikali ya Guatemala, kuvunja ya ndani ya saa 24 mkataba unaoanzisha kamisheni ya kimataifa dhidi ya ukatili nchini Guatemala CICIG.
Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu Guterres amekataa katakata kilichomo katika barua hiyo.
Badala yake amesema Umoja wa Mataifa umekuwa ukizungumza na serikali ya Guatemala kwa ngazi mbalimbali kwa kipindi cha miezi sita iliyopita kwa mujibu wa ibara ya 12 ya makubaliano ya kuunda CICIG ambapo mamlaka ya kamisheni hiyo yamepangwa kufikia ukomo tarehe 3 ya mwezi septemba mwaka huu wa 2019.
“Hadi kufikia tarehe hiyo, tunategemea serikali ya Guatemala kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kisheria chini ya mkataba huo” Guterres amesema kupitia taarifa hiyo.
Katibu Mkuu anatarajia Serikali ya Guatemala kuzingatia shughuli zake za kimataifa ili kuhakikisha ulinzi kwa wafanyakazi wa CICIG, wote wa kimataifa na wa kitaifa.
Katibu Mkuu amekumbushia mchango muhimu wa CICIG katika kupambana na ukatili nchini Guatemala.