Ukosefu wa usalama wachochea wimbi jipya la wakimbizi wa ndani Nigeria
Huko Nigeria imeelezwa kuwa maeneo ya kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo kwenye jimbo la Borno yameshuhudia idadi kubwa ya wimbi la wakimbizi wa ndani katika wiki ya mwisho ya mwaka jana.
Shirika uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limesema wimbi hilo la wakimbizi linafuatia mapigano kati ya vikundi vilivyojihami na jeshi la Nigeria kwenye jimbo hilo.
Takribani wakimbizi wa ndani 8,248 wamewasili katika miji ya Maiduguri, Baga, na Kukawa na tayari wamepatiwa misaada ya kibinadamu ikiripotiwa kuwa wengi wao tangu wamewasili hawana makazi pamoja na huduma za msingi za kujisafi.
Mchanganuo wa taarifa ya IOM unaonyesha kuwa kambi moja huko Maiduguri imepokea kaya 1,517 au jumla ya watu 5,824 ilhali huko Baga jumla ya watu 1,779 wamepatiwa hifadhi.
Katika kambi ya Madinatu kwenye jimbo hilo la Borno wakimbizi wa ndani 1,868 walipokelewa k utoka eneo la Baga ambako hali ukosefu wa usalama imeshamiri.
Wakimbizi hao wa ndani wengi wao wakisema kuwa kata ya Baga huko Kukawa ndio makazi yao ya awali na kilichochochea wakimbie ni mashambulizi kwenye eneo lao sambamba na ukosefu wa usalama.