Wakimbizi wa ndani DRC wafarijika kwa kusaidiana:UNHCR

19 Disemba 2018

Wakati machafuko yakiendelea kusambaratisha familia na kuwalazimisha kufungasha virago nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC maelfu ya wakimbizi wa ndani wanatafuta faraja kwa kusaidiana  kupitia ushirika ulioanzishwa kwa minajili ya kuchagiza ulinzi wa haki za binadamu na kusaka suluhu ya changamoto zinazowakabili 

Jackline Kamala  ni mkimbizi wa ndani nchini DRC, alilazimika kufungasha virago sababu ya vita vinavyoendele Mashariki mwa Congo, alifanikiwa kuokoa watoto wake na kupata hifadhi Kivu ya Kaskazini ambako yeye na maelfu wengine wanahaha kuanza upya maisha yao.

Jackline na wenzie waamua kuanzisha jumuiya ya kusaidiana na yeye ni kiranja wao

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, wakimbizi hawa wa ndani wamepoteza kila kitu na Jackline anatembea mwendo mrefu kukutana na kikundi chake ili kuhakikisha sauti zao zinasikika

Mwaka huu peke zaidi ya watu milioni moja wamekimbia makwao DRC na bado maisha yao yako hatarini. Gloria Ramazani ni afisa wa uhusiano wa nje wa UNHCR

“Wakimbizi wa ndani wanakabiliwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kama vile ukatili wa kingono na kukamatwa kwa nguvu. Mtazamo wa UNHCR ni kuwawezesha watu hawa ili waweze kujitetea na pia kuchukua hatua za ulinzi dhidi ya matukio yanayotokea kwenye jamii yao.”

Anachokitaka Jackline ni jamii na watoto kuwa salama. Hivyo yeye pamoja na wengine wanaojitolea na kwa kupitia msaada wa UNHCR anajaribu kuwapa matumaini watu.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud