Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mtu afahamu kuwa Kakuma kuna vipaji

Pichani iliyopigwa kutoka angani inaonyesha sehemu ya makazi kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya
Picha/Siegfried Modola
Pichani iliyopigwa kutoka angani inaonyesha sehemu ya makazi kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya

Kila mtu afahamu kuwa Kakuma kuna vipaji

Wahamiaji na Wakimbizi

Tamasha la kubaini vipaji lililofanyika kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya, likipatiwa jina “Kakuma’s Got Talent,” yaani ‘Kakuma ina vipaji’ limedhihirisha kuwa kuwa mkimbizi si kukosa kipaji ambapo wakimbizi vijana walionyesha vipaji mbalimbali ikiwemo kuimba, mitindo ya nguo na kucheza. 

Ni video fupi ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbi UNHCR ikianza kwa kuonesha wasichana wawili wakiwa wameshika chupa mithili ya kipaza sauti wakionesha madoido yao ya kucheza.

Baada ya hapo wanaonekana vijana wengi makundi kwa makundi wakionesha vipaji vyao. Wa kucheza ni kucheza kwa bidii yao yote, wa kuimba hali kadhalika.  Jopo la majaji linafuatilia kupima uwezo..

Binti mmoja anasema,“Vijana ambao wako hapa kwenye kambi, ni kizazi kijacho. Tunaweza kufanya kitu katika siku za usoni na tunaweza”

Mmoja wa waandaaji wa mashindano haya Collins Onyango anasema“Kila mtu anatakiwa kufahamu kuwa Kakuma ina vipaji. Kakuma imekuwa hapa tangu mwaka 1992, Leo tunazungumzia zaidi ya wakimbizi 180,000 kutoka nchi 19 tofauti, wana vipaji, maarifa na tofauti pekee ya wao na yeyote aliyeko nje ni kuwa wao walikimbia kuvuka mpaka kuokoa maisha yao”

Fardose Daud msichana mkimbizi kutoka Sudan, anasema amepania kuhakikisha kundi lao la wasichana watupu linashinda, “Watu wengi wanafikiri kila kitu ni cha wavulana. Hata kusakata muziki. Tumeamua mwaka huu tutawaonesha kuwa ambacho anaweza kufanya mwanaume, mwanamke anaweza kukifanya hata vizuri zaidi”

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.