Inasikitisha baadhi ya raia wa DRC hawatashiriki uchaguzi huu muhimu-Bi Zerrougui

28 Disemba 2018

Leila Zerrougui, Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, amesema kuwa anasikitika kwamba kuna raia ambao hawataweza kupiga kura katika uchaguzi mkuu unaofanyika jumapili hii ya tarehe 30 mwezi huu wa Desemba nchini humo, kufuatia uamuzi wa Tume Huru ya Taifaya uchaguzi ya nchi hiyo, CENI, kuahirisha upigwaji kura katika maeneo ya Beni, Butembo na Yumbi kwa sababu ya mlipuko wa Ebola na ukosefu wa usalama.

 

Bi. Zerrougui ambaye ni mkuu wa ujumbe Umoja wa Mataifa nchini humo, DRC,  MONUSCO, akihojiwa hii leo na Radio Okapi ya ujumbe huo amesema, “niliarifiwa kuwa kulikuwa na hili suala kwamba mamia wangepita na kugusa mashine ya kupigia kura, ninaelewa juu ya hofu hiyo. Binafsi ninasikitika kwamba watu wa Beni, Butembo ambao wameteseka sana kwa miaka na vurugu, watu ambao waliuawa wakiwa usingizini, Ebola nayo ilikuwa mateso yao ya pili, hawawezi kupiga kura”

Ameongeza kuwa MONUSCO ilijaribu kusaidia kwa kuweka vifaa vya kusafishia mikono wakati wa kuingia katika vituo vya kupigia kura ili kusaidia kuepuka virusi vya Ebola kusambaa kupitia upigaji kura.

“Wale wanaoandaa wameona kwamba ni hatari na wameamua kuahirisha. Kwa kweli siwezi kusema kwa hakika. Inanisikitisha kwa kuwa ninawachukulia watu wa Beni kuwa ni raia wa DRC na kwamba uchaguzi huu ni wa muhimu na wana haki ya kupiga kura. Na sasa kuna hivi vizuizi, siwezi kusema ni uamuzi mbaya au ni mzuri” amehitimisha Bi. Zerrougui.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter