Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vibali vya kusoma, ajira na familia vyasaidia wakimbizi wengi kuhamia ugenini kihalali- Ripoti

Nchini Italia, mvulana, amesimama nje katika mtaa duni katika mji wa Turin, eneo la Piedmont.
UNICEF/UNI173328/Pirozzi
Nchini Italia, mvulana, amesimama nje katika mtaa duni katika mji wa Turin, eneo la Piedmont.

Vibali vya kusoma, ajira na familia vyasaidia wakimbizi wengi kuhamia ugenini kihalali- Ripoti

Wahamiaji na Wakimbizi

Takwimu mpya zilizotolewa leo zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya nchi wanachama wa ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi OECD, zilipokea wakimbizi wengi kutoka mataifa yenye mizozo kupitia vibali visivyohusiana na masuala ya kibinadamu badala ya mipango ya kuhamishia wakimbizi mataifa mengine.

Kipindi husika ni miaka minane iliyopita na ni kwa mujibu wa takwimu zitokanazo na utafiti wa pamoja wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa  Mataifa, UNHCR na OECD ambao umetolewa leo Geneva, Uswisi ukipatiwa jina Njia salama za wakimbizi.

Takwimu zinaonesha kuwa wakimbizi zaidi ya 560,000 kutoka Syria, Afghanistan, Iraq, Somalia, na Eritrea waliingia nchi wanachama wa OECD kwa kutumia mfumo wa vibali vya kujiunga na familia, kufanya kazi na kusoma.

Idadi hiyo inalinganishwa na wakimbizi 350,400 kutoka mataifa matano ambao waliingia katika kipindi hichocha miaka minane kupitia kupatiwa makazi mpya, idadi ambayo hata hivyo haijumuishi wakimbizi kutoka mataifa matano ambao wamepatiwa hadhi ya ukimbizi au vibali vya kibinadamu kupitia mifumo na kanuni za kusaka hifadhi.

Wakimbizi hao wanafikia milioni 1.5 na waliingia kwenye nchi hizo katika kipindi kimoja, jambo linalotilia mkazo wa  umuhimu wa mfumo bora wa kusaka hifadhi.

Utafiti huo unaonesha kuwa vibali vilivyoongoza kwa wakimbizi kutoka nchi hizo tano kuingia mataifa ya OECD ni zile za kuungana na familia ambazo ni asilimia 86, vibali vya kusoma asilimia 10 ilihali wale wa kusaka ajira ilikuwa ni asilimia 4.

Kaimu Kamishna wa ulinzi wa UNHCR, Volker Türk amesema kuwa licha kuwa njia hizi si mbadala kwa mkimbizi kupatiwa hifadhi taifa lingine, angalau zinatoa fursa kwa mkimbizi kuingia nchi nyingine kihalali na kisheria.

Amesma hatua hiyo sio tu inaweza kusadia wakimbizi kuepuka kutumia njia hatari bali pia itapunguza mzigo kwa mataifa yanayowapokea.

Kwa upande wake mkuu wa masuala ya kazi, ajira na kijamii wa OEDC, Stefano Scarpetta, amesema kuwa katika mukhtadha huu wa dunia wa mmiminiko wa wakimbizi pamoja na kuhama kwa ulazima, njia za familia, kusoma,na vibali vya kufanya kazi vinaweza kutoa mchango mkubwa.

Matokeo ya uchunguzi huu, yatasaidia kuendeleza mpango wa kimkakakti wa miaka mitatu wa mkataba mpya kuhusu wakimbizi kupanua wigo wa kuwapatia wakimbizi makazi mapya.

Takwimu katika ripoti pia zitatumiwa kila mara na UNHCR pamoja na OECD ambazo zitakuwa  watazitoa  kila baada ya miaka miwili.

OECD ina wanachama 36 na asilimia kubwa zinatoka Ulaya ilhali nyingine ni pamoja na Marekani, Japan, Korea Kusini, Chile, Israel na Uturuki.