Azimio la haki za wakulima ni mkombozi kwa kundi hilo lililosahaulika- Bachelet

18 Disemba 2018

Kamishna Mkuu wa  haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amekaribisha hatua ya Baraza Kuu la umoja huo kupitisha azimio la kimataifa kuhusu haki za wakulima na wafanyakazi wa mashambani.

Taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani na Geneva, Uswisi, imemnukuu Bi. Bachelet akisema kuwa “wakulima wanalisha watu wote duniani lakini katu wanashindwa kufurahia haki zao za kibinadamu ikiwemo haki yao ya msingi ya kupata chakula.”

Amesema katika maeneo mengi duniani, wakulima wanakabiliwa na hali ngumu inayochochewa na kutokuwepo kwa mizania kwenye mfumo wa kiuchumi duniani, “sera ambazo zinapaswa kusongesha haki za wakulima hazipo na katika baadhi ya maeneo harakati za kupunguza matumizi zinawaacha taabani.”

Bi. Bachelet amesema kundi lililo taabani zaidi ni wakulima wanawake ambao amesema kutokana na sheria kandamizi na za kibaguzi wanashindwa kupata na kutumia ardhi na zaidi ya yote malipo duni kwa kazi wanayofanya.

Ni kwa mantiki hiyo, Kamishna Mkuu huyo wa haki za binadamu amesema “ni matumiani yangu kuwa azimio hili litasaidia kuongeza azma za serikali katika kuzingatia na kulinda haki na utu wa wakulima na watu wengine wanaofanya kazi mashambani.”

Amesema kundi hilo lina dhima muhimu katika kusongesha na kulinda utamaduni, mazingira, mbinu za kujipatia kipato na mila na hivyo hawapaswi kuachwa nyuma wakati serikali zinatekeleza ajenda ya maendeleo endelevu, SDG.

Azimio hilo lililopitishwa jana Jumatatu, linaongezea uzito kanuni na taratibu za kimataifa zinazohusu haki za watu zaidi ya bilioni moja ikiwemo wakulima, wafanyakazi wa mashambani, wavuvi, wafugaji na makundi mengine kwa kuwapatia mwongozo mahsusi wa kulinda haki zao.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

 

TAGS: Wakulima, Michelle Bachelet, SDGs

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter