Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rebecca Gyumi na washindi wenzake watuzwa UN

Washindi wa tuzo ya haki za binadamu ya UN kwa mwaka 2018 wakiwa na tuzo zao. Wa pili kutoka kulia ni Rebeca Gyumi kutoka Tanzania
UN / Evan Schneider
Washindi wa tuzo ya haki za binadamu ya UN kwa mwaka 2018 wakiwa na tuzo zao. Wa pili kutoka kulia ni Rebeca Gyumi kutoka Tanzania

Rebecca Gyumi na washindi wenzake watuzwa UN

Haki za binadamu

Washindi wa tuzo ya haki za binadamu ya Umoja wa  Mataifa kwa mwaka 2018 hii leo wamepatiwa tuzo hizo kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani.

UN/Priscilla Lecomte
Rebeca!

Washindi hao ambao ni watu watatu akiwemo Rebeca Gyumi kutoka Tanzania, na shirika moja, wamekabidhiwa tuzo hizo wakati wa kikao cha 58 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichoongozwa na Rais wa Baraza hilo Maria Fernanda Espinosa.

Bi.Espinosa ndiye amefungua kikao hicho ambapo kabla ya kukabidhi zawadi amezungumza na kusema kuwa washindi wote wamejikita katika haki za binadamu kuanzia za wanawake, wahamiaji, na ya zaidi ya yote,

"Tuzo hii pia ni ujumbe wa shukrani kwa watetezi wote wa haki za binadamu popote pale walipo, kwasababu kujitoa kwao na kuendelea kupambana kumetuwezesha kuwa na jamii ambayo angalau pengo la kutokuwepo usawa na haki si kubwa. Na kwa washindi wa leo tunaelezea mshikamano nao, na kwamba jitihada zao ni ushahidi kuwa vitendo ni muhimu na kila wakati tunaweza kuleta mabadiliko.”

Kisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akasema kuwa mara nyingi kazi za watetezi wa haki za binadamu ni za hatari wakikumbwa na mauaji, mateso, kutoweshwa na hata kufungwa lakini washindi wamekuwa jasiri akisema, 

"napenda kutoa pongezi kwa Rebeca Gyumi kutoka Tanzania, mwanaharakati wa haki ya elimu kwa wasichana; kwa hayati Asma Jahangir, kutoka Pakistan; kwa Joênia Batista de Carvalho, mwanamke wa kwanza wa jamii ya watu wa asili kuwa mwanasheria; na kwa shirika la Front Line Defenders kutoka Ireland, kwa kufanya kazi kulinda watetezi wa  haki walio hatarini. Kazi zao na zile za watetezi wa haki za binadamu kote duniani ni muhimu kwa jukumu letu la pamoja la kusongesha amani na kuhakikisha maendeleo jumuishi endelevu na heshima ya haki za binadamu kwa wote.”

Joenia Wapichanam mwanamke kutoka jamii ya asili nchini Brazili ambaye naye ameshinda pia tuzo ya haki za binadamu ya UN ya mwaka 2018
Mayra Wapichana
Joenia Wapichanam mwanamke kutoka jamii ya asili nchini Brazili ambaye naye ameshinda pia tuzo ya haki za binadamu ya UN ya mwaka 2018

Na ndipo muda wa tuzo ukawadia…

Tukio hili lilifuatiwa na kikao maalum kwa washindi kuzungumza na kujibu hoja kutoka kwa washiriki ambapo Rebeca Gyumi amesema leo ni wakati wa kujivunia siyo tu yeye bali pia nchi yake Tanzania na jamii yake na kwamba, nahisi kama huu ni ushuhuda kuwa wasichana popote pale walipo; unaweza na mnaweza kuwa chochote kile bila kikwazo, na ni jambo ambalo tumekuwa tunapigania kuweka mazingira ambamo kwayo mtoto wa kike anaweza kuchanua bila kuwa na hofu kuwa siku ijayo mzazi anaweza kuibuka na kukueleza kuwa tumekupatia mume.”

Amesema dunia ambayo mtoto wa kike anaweza kuota ndoto na kufikia bila kikwazo, ndio dunia ambayo yeyé na taasisi aliyoanzisha ya Msichana Intiative ndiyo wanahaha kuifikia Tanzania.

 Washindi wa tuzo hii walitangazwa mwezi uliopita wa Novemba.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.