Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mambo yamekamilika, macho na masikio Marrakech

Bendera za Morocco na ya Umoja wa Mataifa zikipandishwa kwenye eneo la mkutano kuashiria kufunguliwa kwa mkutano wa kupitisha mkataba wa kimatafa kuhusu uhamiaji Marrakech, Morocco
UN /Mark Garten
Bendera za Morocco na ya Umoja wa Mataifa zikipandishwa kwenye eneo la mkutano kuashiria kufunguliwa kwa mkutano wa kupitisha mkataba wa kimatafa kuhusu uhamiaji Marrakech, Morocco

Mambo yamekamilika, macho na masikio Marrakech

Wahamiaji na Wakimbizi

Sasa ni wakati wa kupatia uhai mkataba wa kimataifa kuhusu uhamiaji salama na unaofuata kanuni, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati akizungumza kwenye hafla maalum ilyofanyika huko Marrakech nchini Morocco, wakati wa mkesha wa kuanza mkutano wa viongozi waandamizi wa serikali wenye lengo la kupitisha mkataba huo siku ya Jumanne.
 

Mkutano huo wa siku mbili unaanza kesho mjini Marrakech nchini Morocco ambayo tayari zaidi ya viongozi waandamizi wakiwakilisha zaidi ya serikali na nchi 150 wameshawasili.

Guterres amesema ni lazima kupatia uhai “kile ambacho tumekubaliana na kuonyesha thamani ya mkataba huo kwa serikali wakati zinatunga na kutekeleza sera zao za uhamiaji na pia kwa jamii ambako wahamiaji wanatoka, wanakokuwepo wakati wa mpito wa safari na kule wanakotamatishia safari zao. Lakini pia thamani ya mkataba huo kwa wahamiaji wenyewe.”

Katibu Mkuu amesema moja ya vipengele muhimu vya mkataba huo ni utambuzi wake wa majukumu ya kila mtu, zikiwemo serikali, wahamiaji wenyewe bila shaka, mashirika ya kirai, wasomi, vyama vya wafanyakazi, sekta binafsi, vikundi vya ughaibuni, jamii za wenyewe, wabunge, taasisi za haki za binadamu za kitaifa na vyombo vya habari.

“Umoja wa Mataifa nao utakuwa sehemu ya makundi ya wadau hao na ndio maana tumeamua kuanzisha mtandao wa Umoja wa Mataifa wa uhamiaji. Huu utahamasisha uwezo wetu wote na utaalamu tulio nao katika kuwasaidia ninyi nchi wanachama,” amesema Guterres huku akitaja mambo makuu manne kuhusu mtandao huo.

Amesema mosi, utajikita kwenye ushirikiano, pili shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM litakuwa na dhima kuu. Tatu amesema mtandao huo utakuwa na mfumo jumuishi na kuweza kuchukua  hatua haraka. “Nne mtandao utasaidia nchi wanachama kushirikishana kwenye mikakati badala ya kila moja kuibuka na mpango wake. Na tano mtandao huu utakuwa wazi kujumuisha wadau wa pande zote kwa kuzingatia utofauti uliomo ndani ya Umoja wa Mataifa.”

Mwaklishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji wa kimataifa, Louise Arbour akizungumza na wajumbe wakati wa tukio la kupandisha bendera kwenye eneo la mkutano huko Marrakech Morocco.
UN /Mark Garten
Mwaklishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji wa kimataifa, Louise Arbour akizungumza na wajumbe wakati wa tukio la kupandisha bendera kwenye eneo la mkutano huko Marrakech Morocco.

Mkataba wa uhamiaji wapata jina jipya

Mapema asubuhi, kama ilivyo ada mkutano wa Umoja wa Mataifa unapofanyika kwenye nchi, hufanyika tukio la kupandisha bendera ya nchi husika kwenye eneo la mkutano sambamba na ile ya ile ya Umoja wa Mataifa, kuashiria kuwa sasa eneo hilo limekamilika tayari kuanza kwa mkutano.

Tukio hilo lilishuhudiwa na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya uhamiaji, Louise Arbour na Mwakilishi wa kudumu wa Morocco kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Omar Hilale.

Akizungumza kwenye tukio hilo ambalo ameliita la kihistoria, Bwana Hilale amesema ni la kihistoria kwa sababu mbili, “mosi hii ni mara ya kwanza mkutano wa Umoja wa Mataifa unafanyika Morocco kujadili masuala ya uhamiaji. Pili Nyaraka ya Marrakech itakuwa nyaraka ya kwanza katika historia ya Umoja wa Mataifa kushughulikia haki za wahamiaji na kuzitetea. Hivyo Marrakech itapatia nyaraka hiyo jina lake.”

Kwa upande wake Bi. Arbour amepongeza Morocco kwa kuweka mazingira bora kwa ajili ya upitishaji wa nyaraka hiyo akisema itasalia kuwa rejeleo la siku za baadaye kuhusu mienendo ya binadamu ya uvukaji mipaka.

Awali akizungumza na waandishi wa habari, Bi. Arbour amesema ingawa inaonekana kuna changamoto katika kutekeleza nyaraka hiyo, nchi ambazo zitakuwa tayari kukabiliana na changamoto hizo na kuwa na mtazao chanya zitanufaika nayo.