Mkataba wa kimataifa wa uhamiaji kupitishwa rasmi Marrakech- UN

10 Disemba 2018

Wakuu wa nchi na serikali, mawaziri, viongozi wengine wa ngazi ya juu, asasi za kiraia na wawakilishi toka sekta za umma na binafsi wamekusanyika mjini Marrakech nchini Morocco,   kwa ajili ya mkutano wa ngazi ya juu kwa lengo moja tu, kupitisha mkataba wa kimataifa wa uhamiaji.

Mkutano huo wa siku mbili ulioanza leo na utamalizika kesho Disemba 11 ukiendeshwa na serikali ya Morocco, unafanyika chini ya mwamvuli wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kufuatia makubaliano ya nchi wanachama ya azimio la New York kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji.

Mkataba huo utakuwa wa kwanza kabisa wa kimataifa kwa ajili ya uhamiaji salama, wa mpangilio na wa kawaida.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, Rais wa Baraza Kuu María Fernanda Espinosa na mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kwa ajili ya uhamiaji wa kimataifa Louise Arbour wamefungua mkutano huo na  Bi. Arbour pia ndiye katibu mkuu wa mkutano.

Masuala yanayoambatana na mkutano huu ni pamoja na mijadala kwa siku zote mbili ambapo nchi wanachama wanathibitisha ahadi zao za kisiasa kwa ajili ya mkataba huo wa kimataifa wa uhamiaji.

Wahamiaji wakiandaa samaki kwa ajili ya mauzo katika soko moja mjini Dubai
ILO/Deloche P
Wahamiaji wakiandaa samaki kwa ajili ya mauzo katika soko moja mjini Dubai

Majadiliano hayo yataonyesha njia ya utekelezaji na ushirikiano katika ngazi zote yakishirikisha wadau. Miongoni mwa wanaoendesha majadiliano ni Madeleine Albright waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, Ellen Jonson Sirleaf rais wa zamani wa Liberia na mwenyekiti wa jopo la ngazi ya juu kuhusu uhamiaji wa kimataifa Afrika. Mada zitakazopewa kipaumbele katika mijadala hiyo ni “ushirikino na miradi bunifu katika kusonga mbele”

Historia ya mkataba wa kimataifa kwa ajili ya uhamiajisalama, wa mpango na wa kawaida:

Mkataba wa kimataifa wa uhamiaji ni matokeo ya zaidi ya miezi 18 ya majadiliano na mashauriano miongoni mwa nchi wanachama na wadau wengine wakiwemo viongozi wa kijamii, asasi za kiraia na wahamiaji , kwa kuzingatia azimio la new York ambalo lilipitishwa bila kupingwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi septemba 2016.

Ni makubaliano ya kwanza kabisa ya kimataifa kwenye Umoja huo kuhusu mtazamo wa pamoja wa uhamiaji wa kimatafa na nyanja zake zote.

Wafanyakazi wahamiaji wakiwa kazini katika kiwanda cha matofali huko Mawlamyine, Myanmar.
IOM
Wafanyakazi wahamiaji wakiwa kazini katika kiwanda cha matofali huko Mawlamyine, Myanmar.

Akizungumzia umuhimu wa mkataba huo wakati wa uzinduzi wa ripota yake “Kuufanya uhamiaji kuwa wa manufaa kwa wote” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema “ni fursa ya kutumia mchango ambao tayari  unaotolewa na mamilioni ya wahamiaji katika jamii zetu na kuafikiana hatua za kuchukua kuhakikisha kwamba haki za wahamiaji wote zinaheshimiwa.”

Wakati lengo kuu la mkataba wa kimataifa wa uhamiaji ni kuboresha ushirikiano na udhibiti wa watu kuvuka mipakani , mkataba huo pia unaweka bayana kwamba haumfungi yeyote kisheria na unaheshimu uhuru.

Malengo muhimu ya mkataba:

Mtakaba huo unaorodhesha malengo 23 ya kusaidia kudhibiti uhamiaji katika ngazi zote , kimataifa, kitaofa na kijamii. Miongoni mwa malengo hayo ni kushughulikia masuala kamasababu zinazowazuia watu kuwa na maisha endelevu katika nchi zao za asili , hatari zinazowakabiliwatu katika hatua zote za uhamiaji, hofu za serikali na jamii, athari za kiuchumia na kijamii zitakazowakumba wahamiaji  na athari za kijamii na kimazingira zinazotokana na uhamiaji wakati jamii zikipitia mabadiliko, lakini pia juhudi za kuweka mazingira ya kusaidia wahamiaji kuleta faida katika jamii kupitia mchango wao wa kiutu, kiuchumi na kijamii kwa maendeleo endelevu.

Kila lengo katika mkataba huo ni muhimu na mkataba unatoa orodha na hatua zinazoweza kuchukuliwa ambazo serikali zinaweza kuzitumia ili kuanzisha mikakati yao ya utekelezaji wa sera zao za uhamiaji.

Hatua hizi zinatokana na mifano mizuri ya kimataifa ya kukabiliana na uhamiaji na mafunzo yaliyojitokeza ambayo yalikusanywa wakati wa mchakato wa majadiliano ya mkataba huo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter