Sera za  uhamiaji zinazofaa mtoto na kijana, zamfaa kila mtu- UNICEF

10 Disemba 2018

Kufuatia kupitishwa hii leo huko Marrakech nchini Morocco, mkataba wa kimataifa kuhusu uhamiaji salama, unaofuata kanuni na wa kawaida, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema hatua hiyo ya kihistoria ni mafanikio kwa wahamiaji watoto na serikali.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa hii leo New York, Marekani na huko Marrakech, imesema “kwa mara ya kwanza, watoto wanatambuliwa kuwa kitovu cha usimamizi wa uhamiaji. Bila kuweka wajibu mpya, mkataba unapatia serikali mbinu muhimu ya kusaidia kukidhi wajibu wa kisheria uliopo wa kulinda, kujumuisha na kuwezesha watoto wote.”

Halikadhalika imesema mkataba huo pia unasaidia mamilioni ya watoto na vijana walioathiriwa na uhamiaji kuweza kuchanua kwa kadri ya uwezo wao.

Sambamba na hilo, serikali zitaweza kushughulikia vyanzo vya watoto kukimbia makwao na kuwapatia watoto wahamiaji fursa nzuri zaidi ya elimu pamoja na huduma za afya na ulinzi dhidi ya ukatili pamoja na kuweka familia pamoja.

Hata hivyo UNICEF inasema ni ajabu kuwa  “leo hii, zaidi ya nchi 100 bado zina sera za kuwa na vituo vya kuwasweka rumande watoto wahamiaji. Hebu fikiria iwapo dunia ingepitisha kwa pamoja uwepo wa vituo mbadala badala ya hivyo vya kushikilia watoto wahamaiji, idadi ya watoto wanaoshikiliwa kwenye vituo vya uhamiaji ingalipungua kutoka milioni hadi sifuri.”

UNICEF México
Watoto ni miongoni mwa wahamiaji kutoka Amerika ya Kati ambao wanatembea kuelekea Marekani. Pichani ni mmoja wa watoto waliokuwa wamepigwa picha kwenye mitaa ya Tapachula, Chiapas nchini Mexico tarehe 21 Oktoba 2018

Changamoto hivi sasa kwa mujibu wa UNICEF ni kuchukua  hatua inayofuata ambayo ni kusonga mbele zaidi badala ya kutambua tu hatari zinazokumba watoto wahamiaji, “tuongeze dhima zao katika kuchochea maendeleo na ustawi wao. Tunahitaji kufanya kazi bora zaidi ya kuwashirikisha na kusikiliza sauti zao, mahitaji yao, hofu zao na matamanio kuhusu mustakabali wao.”

Kwa mantiki hiyo UNICEF inataka watoto na vijana siyo tu waweze kuwa sehemu ya suluhu ya uhamiaji bora bali pia lazima wawe suluhu ya kuhakikisha  uhamiaji ni salama kwa kila mtu.

Ikimnukuu mmoja wa wajumbe vijana huko Marrakech, aitwaye Yasmin, UNICEF imesema sera za uhamiaji ambazo zinafaa kwa vijana na watoto zinafaa kwa kila mtu kwa hivyo imesema iko tayari kushirikiana na serikali kusaidia utekelezaji wa nyaraka hiyo.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud