Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubia mpya walenga kusaka suluhu ya kudumu dhidi ya ukimbizi wa ndani

Mkimbizi wa Rohingya kutoka Myanamr, akiwa ameketi na watoto wake wawili kati ya wanne katika malazi yao kwenye kambi ya Nayapara Kusini Mashariki mwa Bangladesh 22 Oktoba 2018.
© UNHCR/Chris Melzer
Mkimbizi wa Rohingya kutoka Myanamr, akiwa ameketi na watoto wake wawili kati ya wanne katika malazi yao kwenye kambi ya Nayapara Kusini Mashariki mwa Bangladesh 22 Oktoba 2018.

Ubia mpya walenga kusaka suluhu ya kudumu dhidi ya ukimbizi wa ndani

Wahamiaji na Wakimbizi

Harakati za kusaka suluhu kwa makumi ya mamilioni ya watu waliojikuta ni wakimbizi ndani ya nchi zao kutokana na mizozo na majanga ya kiasili zitapatiwa nguvu mpya kufuatia makubaliano mapya yaliyotiwa saini hii leo huko Geneva, Uswisi kati ya shirika la uhamiaji la Umoja wa mataifa, IOM na kituo cha kufuatilia ukimbizi wa ndani, IDMC.

Ubia huo  utasaidia kusongesha sera za kitaifa na kimataifa kwa lengo la kuboresha maisha ya wakimbizi wa ndani duniani kote, kwa kuzingatia ubobezi wa IDMC katika uchambuzi wa data za ukimbizi wa ndani, utafiri na utungaji wa sera.

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa IOM Antonio Vitorino amesema harakati za shirika lake kwa maslahi ya wakimbzi wa ndani kwa lengo la kusaidia nchi wanachama, ni moja ya kazi yao kubwa zaidi duniani kote na kwamba, “ubia huu utasongesha mbele zaidi ubora wa kazi hiyo na kutuwezesha kuhamasisha hatua zaidi kwa suala hili ambalo halijapatiwa kipaumbele cha kutosha.”

Ushirikiano huo kati ya IOM na IDMC unakuja wakati ukimbizi wa ndani unazidi kushika kasi kutokana na ukosefu wa utulivu ndani ya nchi, licha ya misingi ongozi ya Umoja wa Mataifa kuhusu ukimbizi wa ndani ikitimiza miaka 20 tangu kuasisiwa.

IOM inasema idadi ya wakimbizi wa ndani hivi sasa imeongezeka maradufu tangu mwaka 2000, kasi kubwa ya kuongezeka ikiwa ni miaka mitano iliyopita.

“Pamoja na watu milioni 40 ambao wamekuwa wakimbizi wa ndani kutokana na migogoro, watu wengine milioni 18.8 walikuwa wakimbizi wa ndani mwaka 2017 kutokana na majanga yahusianayo na mabadiliko ya tabianchi,” imesema IDMC.

Mkurugenzi wa IDMC Alexandra Bilak akizungumzia hali hiyo amesema “bado kuna mapengo mengi katika jinsi tunavyoelewa na kushughulikia tatizo hili. Changamoto na fursa za hali ya sasa ya ukimbizi wa ndani vinahitaji mwelekeo wa kimkakati na ubia huu unatupatia fursa ya ushawishi wa kisiasa tunaohitaji ili kusongesha mbele kazi  yetu, kuendeleza mwelekeo mpya na kusaidia serikali kusaka suluhu ya kudumu kwa suala hili.”

Kwa mantiki hiyo, IOM na IDMC wataandaa mkakati wa pamoja wa kusaka rasilimali zinazohitajika kutekeleza mipango  yao na kushirikiana ili kuwa na mifumo ya kina zaidi dhidi ya ukimbizi wa ndani.