Wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa wakumbusha msaada wa dharura kwa wakimbizi warohingya Bangladesh

Kamishna Mkuu wa wakimbizi duniani, Filippo Grandi (kushoto) akikutana na wafanyakazi wa UNHCR na wakimbizi kutoka Myanmar kwenye kituo cha usajili huko kambini Kutupalong nchini Bangladesh
© UNHCR/Will Swanson
Kamishna Mkuu wa wakimbizi duniani, Filippo Grandi (kushoto) akikutana na wafanyakazi wa UNHCR na wakimbizi kutoka Myanmar kwenye kituo cha usajili huko kambini Kutupalong nchini Bangladesh

Wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa wakumbusha msaada wa dharura kwa wakimbizi warohingya Bangladesh

Wahamiaji na Wakimbizi

Umoja wa Mataifa umesisitiza ari yake kuendelea kuhakikisha usalama na suluhu ya kudumu kwa wakimbizi warohingya kutoka Myanmar na kukumbusha juhudi za Umoja huo katika kuweka mazingira salama kuwawezesha kurejea nyumbani.

Kupitia taarifa ya pamoja, wakuu wa mashirika matatu ya Umoja huo baada ya ziara ya pamoja nchini Bangladesh wametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuendelea kusaidia mahitaji muhimu ya watu milioni 1.2 kusini mashariki mwa Bangladesh hususan wakimbizi warohingya lakini pia jamii zinazowahifadhi.

Wakuu hao akiwemo Mark Lowcock, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, mkurugenzi mkuu wa Shirika la uhamiaji, IOM António Vitorino na kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi baada ya ziara yao huko kwenye kambi za wakimbizi Cox’s Bazar na kukutana na wakimbizi, wamesisitiza umuhimu wa kusaidia wakimbizi waliiokimbilia nje ya nchi na hususan kuimarisha fursa za kusoma na mafunzo ya stadi mbali mbali.

Kwa mujibu wa taarifa yao, nusu ya watoto wakimbizi 540,000 chini ya umri wa miaka 12 hawahudhuri shule huku idadi iliyosalia ikiwa na fursa ndogo tu ya kupata elimu n ani watoto wachahe tu barubaru wana uwezo wa kupata elimu au mafunzo.

“Hii inasalia kuwa janga kubwa ya wakimbizi, kuna zaidi ya wakimbizi 900,000 warohingya walioko Bangladesh wengi wa waliokimbia Myanmar 2017”, amesema bwana Grandi. Ameongeza kuwa, “Nimeona hatua kubwa zilizopigwa, lakini hali ya wakimbizi hususan wanawake na watoto bado ni mbaya. Wakati tukishuhudia janga la hivi sasa miaka miwili baadaye ni lazima tuwape wakimbizi fursa ya kusoma, kujenga stadi na kuchangia katika jamii wakati tukiwaandaa kurejea Myanmar, mustakabali wa wakimbizi warohingya uko njia panda.”

Nchini Bangladesh wakimbizi kutoka Myanmar ambao ni kabila la warohingywa wakiwa wamesaka hifadhi kwenye eneo la Cox's Bazar
© UNHCR/Santiago Escobar-Jaramillo
Nchini Bangladesh wakimbizi kutoka Myanmar ambao ni kabila la warohingywa wakiwa wamesaka hifadhi kwenye eneo la Cox's Bazar

Kwa upande wake Bwana Vitorino amesema, “jamii ya warohingya inajumuishwa na vijana wengi ambao wanahitaji kupewa matumaini na fursa iwapo watajenga maisha bora baada ya kurejea Myanmar.”

Kwa upande wake Bwana Lowcock amesema, “mara ya kwanza nilipokuja Cox’s Bazar mwaka 2017, mamia ya maelfu ya warohingya walikuwa wamekimbilia mpakani kukimbia ukatili usioelezeka, nilikutana na watoto waliokuwa wameshuhudia wazazi wao wakiuawa. Wanawake walisimulia vitendo vya ukatili wa kingono na walivyonusurika.”

Ameongeza kwamba, “wakati wa ziara hii tumekutana na wanaume wakimbizi ambao ni mfano wa kuigwa pamoja na wanawake wanaojitolea walionusurika ukatili na wanaosaidia kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinisia na wa kingono kambini.”

Bwana Lowcock ametoa pendekezo akisema, “njia mujarabu ni kusaidia wakimbizi sio tu kuibuka kutokana na machungu waliyoyapitia lakini pia kuwaanda kkwa ajili ya mustakabali wenye hadhi.”

Ziara ya wakuu hao imefanyika wakati huu ambapo kunatarajiwa kimbunga ambacho kinafuatiwa na upepo mkali, huku vyote vikiweka hatari kubwa ikiwemo, mafuriko, tetemeko la ardhi, milipuko ya magonjwa kwa maelfu ya wanawake, wanaume na watoto ambao wako hatarini.

Wakuu hao wamejadili na serikali kuhusu mbinu ambazo jamii ya kimatafia inaweza kusaidia maandalizi na juhudi za kukabiliana na hali iliyopo.

Viongozi  hao wakiwa ziarani wameshuhudia mazingira magumu ambako wakimbizi walikimbia na kutiwa moyo na ustahimilivu wao.

TAGS: Mynamar, Cox's Bazar, Mark Lowcock, António Vitorino, Filippo Grandi, Rohingya