Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM na wadau wajadili usalama wa wakimbizi na wahamiaji Ubelgiji.

Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediteranea
Italian Coastguard/Massimo Sestini
Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediteranea

IOM na wadau wajadili usalama wa wakimbizi na wahamiaji Ubelgiji.

Wahamiaji na Wakimbizi

Mkutano wa kwanza wa nchi wanachama wa Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM), kuhusu mbinu jumuishi za uhamiaji na kuoanisha njia za wahamiaji kwenda Ulaya, umefanyika mjini Brussels, Ubelgiji na kuleta matumaini kwa mashirika yanaohusika na wakimbizi na wahamiaji.

Mkurugenzi Mkuu wa IOM, António Vitorino, amesema uwepo wa suluhisho za kibinadamu kukabiliana na changamoto ambazo zinawakumba watu wanaolazimika kuhama ni muhimu kwa kuzingatia kiwango cha waathirika.

Amesema kwa sasa kuna watu milioni 68.5 waliolazimika kuhama makwao duniani kote.

Bwana Antonio alionyesha matumaini kuwa mengi zaidi yanaweza kufanywa kuhusu uhamiaji na njia za wahamiaji kupitia endapo kuna ushirikiano kusaidia wakimbizi na wahamiaji walio hatarini.

IOM imezipongeza nchi za Canada, Argentina, Chile na Muungano wa Ulaya kwa kupanua mipango yake ya kukubali wahamiaji kwa msingi wa utu katika miaka ya hivi karibuni na kuendelea kuanzia njia salama wanakopitia wakiingia nchi hizo.

Eugenio Ambrosi, Mkuu wa wahudumu wa IOM ambaye pia ni Mkurugenzi wa kanda la Mungano wa Ulaya, Norway na Switzerland amesema kujadili uhamiaji na ulinzi wa ziada sio tu jukwaa la michakato na taratibu, bali pia inatoa fursa za kubadilisha maisha na ulinzi wa binadamu wenzetu walio katika uhitaji.

Pia alitoa wito kwa wanaharakati wote kushirikiana kufanya kila wawezalo kuhakikisha ubora wa maisha ya watu hao.

Wawakilishi wa nchi 25 za Ulaya na wadau wao kutoka Australia, Asia, Amerika Kaskazini na Kusini wamehudhuria mkutano huo pamoja na maafisa kutoka taasisi mbalimbali za Ulaya.