Skip to main content

UNHCR yapelekea maelfu ya mahema kwa waathirika wa ukame Afghanstan

Awali, WHO kwa kusaidiwa na UNICEF iliwapa chanjo ya Polio watoto wa kusini mwa Afghanstan.
UNICEF/Celeste Hibbert
Awali, WHO kwa kusaidiwa na UNICEF iliwapa chanjo ya Polio watoto wa kusini mwa Afghanstan.

UNHCR yapelekea maelfu ya mahema kwa waathirika wa ukame Afghanstan

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi, UNHCR, limeanza kazi ya kupeleka kwa ndege  mahema kwa maelfu ya raia wa Afghanistan walioko Magharibi mwa nchi hiyo ambao wamekuwa wakimbizi wa ndani ya nchi yao kwa sababu za ukame pamoja na vita vinavyoendelea nchini humo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva Uswisi, msemaji wa UNHCR, Babar Baloch, amesema zoezi hilo lililoanza mwishoni mwa juma litaendelea hadi kila anayehitaji msaada huo kufikiwa.

Ameongeza kuwa vita vinavyoendelea na ukame uliokithiri vimeshuhudia robo milioni ya raia wa Afghanistan wakitawanywa  nchini humo tangu mwezi April mwaka huu. Hadi sasa takriban familia 220,000 zinaishi katika vibanda vya kujishikiza katika mikoa ya Magharibi mwa Afghanistan ya Herat, Badghis na Ghor. Hali yao inazidi kuwa mbaya kutokana na kukaribia kwa majira ya baridi na tayari kumeanza kushuhudiwa ongezeko la vifo vya watoto.

Ndege 12 za UNHCR zinafanya safari hizo za kusafirisha mahema ambapo kufikia sasa wameshasafirika na kugawa mahema 15,100 kwa lengo la kuwapunguzia madhila takriban nusu ya watu waliotawanywa. Mahema hayo ambayo yanasafirishwa kutoka Pakistan ni sehemu ya msaada mkubwa  ulioandaliwa kwa ushirikiano wa serikali ya Afghanistan na washirika wake . Kwa sababu watu wengi wasio na makazi wako katika ardhi ya watu binafsi na wanaweza kufurushwa mda wowote ule, UNHCR inasaidia juhudi za serikali kutafuta ardhi ambako watu hao watapatiwa makazi.