Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio Afghanistan ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa za haki:UN

Mazishi ya raia waliouawa kwenye shambulio la kujitoa muhanga mjini Kabul , Afghanistan Juni 2018. Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNAMA uliripoti kuwa idadi kubwa zaidi ya watu waliuawa kufikia nusu ya mwaka huu wa 2018.
Fardin Waezi/UNAMA

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio la leo nchini Afghanistan lililowalenga watu waliokusanyika kusheherekea siku muhimu ya kidini.

Kufuatia taarifa iliyotolewa na msemaji wake , Antonio Guterres amesema  kuwalenga raia kwa makusudi ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na kusisitiza kila juhudi zifanywe kuhakikisha wahusika wa shambulio hilo wanafikishwa mbele ya mkono wa sheria.

Duru za habari zinasema mshambuliaji wa kujitoa muhanga alijilipua kwenye mkusanyiko mkubwa wa watu mjini Kabul, shambulio lililokatili maisha ya watu 50 na kujeruhi wengine zaidi ya 70. Watu hao ambao wengi ni Waislam wa madhehebu ya Sunni wakijumuisha viongozi wa dini na wanazuoni walikuwa wamekusanyika kuadhimisha sikukuu ya Maulid ambayo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa mtume Mohammad.

Na wajumbe katika hafla hiyo wametoka katika sehemu mbalimbali za Afghanistan. Hafla hiyo iliandaliwa na Baraza la Ulema afghanistan ambacho ni chombo kikubwa cha kidini nchini humo.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika wa shambulio hilo na serikali ya Afghanistan. Pia amewatakia afuweni ya haraka majeruhi.