Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Afghanistan wako hatarini zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote:UNICEF

Ni moja ya tano ya wasichana walio chini ya umri wa miaka 15 ndio wanaojua kusoma na kuandika Afghanistan
© UNICEF/Frank Dejo
Ni moja ya tano ya wasichana walio chini ya umri wa miaka 15 ndio wanaojua kusoma na kuandika Afghanistan

Watoto Afghanistan wako hatarini zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote:UNICEF

Amani na Usalama

Chondechonde hatuwezi kuwatelekeza sasa watoto wa Afghanista kwani mahitaji yameongezeka zaidi  kuliko hapo awali, amesihi afisa mwandamizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) leo baada ya kuhitimisha ziara yake nchini humo.

George Laryea-Adjei, ambaye ni mkurugenzi wa kanda ya Kusini mwa Asia wa UNICEF ameongeza kuwa "Vijana na watoto wamekuwa wakituambia wanahitaji haraka sana vitu vya msingi na huduma mahitaji ambayo endapo msaada utatolewa, jamii ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu inaweza kuyashughulikia kwa urahisi. Mahitaji ya watoto wa Afghanistan hayajawahi kuwa makubwa zaidi kuliko wakati huu. Hatuwezi kuwatelekeza sasa.”

Wanalipa gharama

Watoto wamelipa gharama kubwa zaidi katika wiki za hivi karibuni za kuongezeka kwa mizozo na ukosefu wa usalama, amesema Bwana Lyeye-Adjei, ambaye anaishi nchini Nepal.

Ameongeza kuwa sio tu kwamba wengine wamelazimishwa kukimbia majumbani mwao, na kushindwa kuhudhuria shule zao na kuwa na marafiki zao, pia wamenyimwa huduma za msingi za afya ambazo zinaweza kuwalinda dhidi ya magonjwa kama polio, pepopunda na magonjwa mengine.

"Sasa, kutokana na shida ya usalama, kumekuwa na ongezeko kubwa la bei ya chakula, ukame mkali, kuenea kwa janga la COVID-19, na msimu mwingine wa baridi kali unakaribia, hivyo watoto wako katika hatari zaidi kulikowakati mwingine wowote.” Ameonya afisa huyo.

Msichana wa umri wa miaka 10 akiwa amesimama kwenye kifusi ambapo awali palikuwa ni sehemu ya shule ya wasichana ambayo iliharibiwa wakati wa mlipuko wa bomu mwaka 2015 kwenye kijiji cha Bodyalai
© UNICEF/Marko Kokic
Msichana wa umri wa miaka 10 akiwa amesimama kwenye kifusi ambapo awali palikuwa ni sehemu ya shule ya wasichana ambayo iliharibiwa wakati wa mlipuko wa bomu mwaka 2015 kwenye kijiji cha Bodyalai

Tishio la utapiamlo linanyemelea

UNICEF imetabiri kwamba ikiwa hali ya sasa itaendelea, Watoto milioni moja chini ya miaka mitano nchini Afghanistan watakabiliwa na utapiamlo mkali, ambayo ni hali ya kutishia maisha.

Zaidi ya watoto milioni nne, ikiwa ni pamoja na wasichana milioni 2.2, pia hawaendi shule.

Karibu vijana 300,000 wamelazimika kukimbia makazi yao, ambao wengine walikuwa kitandani wakilala, ghasia zilipozuka "na wengi wao wameshuhudia matukio ambayo hakuna mtoto anayepaswa kuona," Bwana Laryea-Adjei amesema.

"Watoto na vijana wanapambana na msongo wa mawazona hofu, wanahitaji sana msaada wa afya ya akili," akaongeza.

Msaada lazima uongezwe

Kukiwa na washirika wengine wa kibinadamu wanaofikiria kukata misaada kwa Afghanistan, Bwana Laryea-Adjei ameonyesha wasiwasi juu ya kuwa na rasilimali za kutosha kuhakikisha vituo vya afya vinaendelea, shule zinafunguliwa, na kupatikana kwa huduma za kutibu watoto wenye utapiamlo.

UNICEF, ambayo imekuwa Afghanistan kwa zaidi ya miongo sita, inaendelea kudumisha uwepo wake kote nchini, na inashirikiana na wadau wengine kuongeza hatua za msaada.

Shirika hilo kwa sasa linasaidia timu za afya na lishe zinazotembea kwenye kambi za watu waliotawanywa, na kuweka maeneo rafiki kwa watoto, vituo vya lishe na maeneo ya chanjo, wakati pia ikitoa vifaa vya ziada vya kuokoa maisha na kusaidia maelfu ya wanafunzi katika madarasa ya elimu yaliyoko kwenye jamii.

Hata hivyo Bwana Laryea-Adjei amesisitiza kuwa rasilimali zaidi zinahitajika sana. 

Hivi karibuni UNICEF ilizindua ombi la dola milioni $ 192 kushughulikia mzozo wa kibinadamu unaoongezeka, na limewahimiza wafadhili kuongeza msaada wao.