Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu bora ya umma bure ni haki ya msingi, kila nchi inatakiwa kuhakikisha hilo:DSG

Watoto wakicheza nje baaa ya siku ya kusoma Nepal vijijini
Aisha Faquir/World Bank
Watoto wakicheza nje baaa ya siku ya kusoma Nepal vijijini

Elimu bora ya umma bure ni haki ya msingi, kila nchi inatakiwa kuhakikisha hilo:DSG

Utamaduni na Elimu

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed  akizungumza katika mkutano wa sita wa dunia kuhusu elimu uliofanyika Nepal, ameitaka jumuiya ya kimataifa kupanga vizuri rasilimali za kuhakikisha elimu bora inayowahusisha watu wote inamfikia kila mtu.

Bi. Amina amehamasisha kuhusisha faida za utandawazi katika kuhakikisha kutokuwepo kwa usawa hakupewi nafasi zaidi, aidha  akasisitiza kuwa ajenda ya mwaka 2030 kwa ajili ya maendeleo endelevu ni kuiboresha dunia na kila mtu anatakiwa kutimiza ahadi hii.

Bi. Amina ameyasema hayo akihitimisha ziara yake ya siku mbili nchini Nepal ambako pamoja na kuhudhuria mkutano huo wa dunia kuhusu elimu, amekutana na viongozi wa serikali ya nchi hiyo.

Kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Nepal, Bi Amina Mohammed akiwa Kathmandu alifanya mikutano muhimu na viongozi wa serikali ya Nepal akiwemo rais wa nchi hiyo Bi. Bidhya Deva Bhandari. 

Katika mkutano huo, Bi Amina amepongeza maendeleo ya Nepal katika kuelekea amani akisema kuwa utawala bora na taasisi imara ndiyo msingi wa maendeleo endelevu.

Aidha taarifa imeeleza kuwa katika ziara hii naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemtembelea waziri mkuu wa Nepal, KP Oli na wakazungumzia ushirikiano baina ya nchi hiyo na Umoja Mataifa katika maendeleo endelevu wakijikita zaidi katika suala la elimu. 

Bi Amina amesisitiza kuwa kuipata elimu bora ya umma bila malipo ni haki ya msingi na kila nchi inatakiwa kuhakikisha hilo kwa wananchi wake na akaipongeza serikali ya Nepal kwa kulisimamia hilo la haki ya kupata elimu.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametembelea pia  makao makuu ya jeshi la nchi hiyo na kukutana na mkuu wa majeshi Jeneral Purna Chandra Thapa. 

Wakati wa mkutano wao Bi Amina ameisifu Nepal kwa mchango wake katika kutunza amani ya dunia kupitia  kuchangia vikosi katika operesheni za ulinzi wa amani za umoja wa mataifa kwani Nepal ni nchi ya tano kwa uchangiaji mkubwa wa vikosi vya ulinzi wa amani.