Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu yasalia mtihani mkubwa kwa watoto wa kipalestina wasomao maeneo yanayokaliwa na Israel

Shule ya Qurtoba ndani mwa eneo linalolindwa na jeshi la Israel katika H2 Hebron, Ukingo wa magharibi mwa Mto Jordan. Mahala pa kuingilia.
UNRWA/Marwan Baghdadi
Shule ya Qurtoba ndani mwa eneo linalolindwa na jeshi la Israel katika H2 Hebron, Ukingo wa magharibi mwa Mto Jordan. Mahala pa kuingilia.

Elimu yasalia mtihani mkubwa kwa watoto wa kipalestina wasomao maeneo yanayokaliwa na Israel

Amani na Usalama

Huko Ukingo wa magharibi mwa mto Jordan, suala la mtoto wa kipalestina kwenda shule zilizoko kwenye maeneo yanayolindwa na jeshi la Israel ni shughuli kubwa inayoambatana na ukaguzi wa kina, jambo ambalo husumbua watoto hao  kisaikolojia. Mwandishi wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa aliyetembelea eneo hilo hivi karibuni ameshuhudia zahma inayokumba takribani wanafunzi 163 wa shule ya Qurtuba pamoja na walimu wao. 

 

Ni lango la chuma katika kizuizi cha barabarani cha Israel, likifunguliwa katika eneo la H2 kuekelea Hebron mji ambao  asilimia 20 ya wakazi wake 40,000 ni  wapalestina, huku wakiwepo pia waisraeli wachache. Makazi ya waisraeli hawa lina ulinzi mkali unaofanywa na jeshi la Israel kwa kipindi cha miaka mitatu sasa kufuatia mashambulio kadhaa dhidi ya wa Israel.

Baada ya kujitambulisha na kujieleza kwa kina wanafunzi walikubaliwa kusonga mbele hadi shuleni iliyojengwa katika kilima mkabala na makazi ya Beit Hadassah.

 

Shule ya Qurtoba Hebron H2, ukingo wa magharibi wa mto Jordan
UNRWA/Marwan Baghdadi
Shule ya Qurtoba Hebron H2, ukingo wa magharibi wa mto Jordan

Aisha Al Azzah mwanafunzi mwenye umri wa miaka13 anasema wanataka uhuru kwani wamechoshwa na wanachopitia kila siku

‘Maisha yetu hapa ni magumu.Tunateseka kweli kwani kila tunapokuja shuleni tunapofika kwenye vizuizi tunakaguliwa na tena kufanyiwa fujo na walowezi. Siku moja mlowezi mmoja alitusimamisha barabarani na kuanza kutusukumasukuma huku akipiga kelele akituambia ‘ondokeni hapa’ lakini sisi tulimwambia kuwa hatuondoki.”

Naye  mkurugenzi wa shule hiyo,Noura Nassar, ambaye ameongoza shule hiyo kwa kipindi cha miaka sita sasa ameeleza kisa kimoja kilichomsababishia majeraha yeye na  baadhi ya wanafunzi.

“Tukishirikiana na wizara ya kilimo, tuliandaa siku ya kupanda miti kuzunguka shule. Tulishangaa pale kundi la walowezi lilipotushambulia na kutukataza kupanda miti. Baadhi ya watoto walijeruhiwa , na nilikuwa nawasaidia kuwapeleka hospitalini na huko niligunduwa kuwa nami nilijeruhiwa.”

Umoja wa Mataifa unasema kuwa maisha ya wapalestina walioko katika maeneo ya misukosuko ni ya shida kwa kuwa ni vigumu sana kupata mahitaij muhimu.