WFP kuongeza msaada kwa walioathirika na ukame Afghanistan.

16 Novemba 2018

Kutokana na ukame unaoendelea kukumba Afghanistan na kusababisha ongezeko la idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula, serikali ya Afghanisan na mashirika ya Umoja wa Mataifa wanahitaji kupatiwa fedha zaidi ili kukidhi mahitaji hayo, limesema shirika la mpango wa chakula duniani, WFP.

Msemaji wa WFP Herve  Verhoosel amesema hayo leo mjini Geneva, Uswisi wakati akizungumza na waandishi wa habari akisema kuwa “ukame mkali uliathiri majimbo 20 ya kaskazini, kusini na magaribi mwa Afghanistan kati ya majimbo 34 nchi nzima. Majimbo matano miongoni mwa yaliyoathirika zaidi ni Badghis, Ghor, Jawzjan, Faryab na Herat.”Amesema baada ya tathmini iliyofanywa na serikali ya Afghanistani kuhusu uhakika wa chakula, ripoti ya mwisho ya tahmini iliyofanyika kuanzia mwezi Agosti hadi Septemba itatolewa hivi karibuni, lakini matokeo ya awali yanaonesha kuwa watu milioni 3.5 wana uhitaji mkubwa wa msaada wa kibinadamu katika majimbo 20 yaliyoathirika zaidi.

Verhoosel ameongeza kusema kuwa WFP litaongeza msaada wake kufikia watu milioni 2.5 katika maeneo yalioathirika na ukame angalau kwa miezi sita.

Tayari WFP imekuwa ikiwasaidia watu milioni 1.4 kufikia katikati mwa mwezi huu wa Novemba. Wengine milioni moja walioorodheshwa katika tathimini ya uhakika wa chakula, watasaidiwa na serikali ya Afganistani na mashirika mengine yasiyo ya kisekali.

Katika msimu wa kiangazi WFP iliwapatia msaada wa chakula zaidi ya watu laki tano katika majimbo hayo kuanzi mwezi Julai hadi Septemba.

Kufikia mwishoni mwa mwezi Novemba WFP inapanga kuwafikia watu milioni 1.7 na kutoka hadi Machi WFP inapanga kuwafikia watu milioni 2.5 waliolengwa pia inakusudia kuwasaidia watu wenye njaa kubaki katika makazi yao na kujikita katika msimu ujao wa kilimo na pia kuzuia watu kukosa makazi mijini wakati wa baridi kali.

Aidha Verhoosel amesema kuwa WFP pia ina mpango wa kuendelea kuyasaidia maeneo yaliyoathirika kwa ukame kwa kuanzisha miradi. “Nchini kote zaidi ya kilomita 1500 ya mifereji ya kumwagilia imejengwa, miti milioni 10 imepandwa na zaidi ya kilomita 1600 za barabara za vijijini zimeboreshwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita,” amesema.

Serikali ya Afghanstani imechangia tani elfu 60 za ngano kwa WFP kupitia hifadhi ya chakula ya serikali ikiwa ni sehemu ya usaidizi kwa wenye uhitaji.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter