Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tupunguze kiwango cha uchafuzi wa hewa kwa theluthi mbili ifikapo 2030-WHO

Uchafuzi wa hewa kutoka kiwanda nchini Romania.(Picha:UM/R Markli)

Tupunguze kiwango cha uchafuzi wa hewa kwa theluthi mbili ifikapo 2030-WHO

Afya

Mkutano wa kwanza wa kimataifa kuhusu uchafuzi wa hali ya hewa na afya umemalizika kwa shirika la afya ulimwenguni, WHO kupendekeza kupunguzwa kwa theluthi mbili kwa kiwango cha uchafuzi wa hali ya hewa ifikapo mwaka 2030.

Dkt. Maria Neira, Mkurugenzi wa Idara ya afya ya  umma na mazingira WHO, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo pendekezo hilo ni fursa njema na kwamba watahamasisha kila mtu kufanikisha pendekezo hilo wakati huu ambapo idadi ya watu wanaofariki dunia kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa ni milioni 7.

Mkurugenzi huyo amesema WHO itatumia mbinu zake na kwamba..

“Kwa nchi zilizoendelea zaidi tutapunguza kiwango cha  hewa ya chafuzi kinachotolewa kwenye mfumo wa afya na kwa nchi ambako mfumo wa afya hauchangii kabisa kwenye hewa chafuzi, zinahitaji kuwa na umeme na chanzo salama cha nishati. Tutalenga kuweka mfumo wa umeme pia ifikapo mwaka 2030.”

Ameongeza kuwa ni lazima sekta ya afya ipaze sauti kuhakikisha kwamba mapendekezo hayo yanafanikiwa akigeukia pia watu bilioni 3 ambao bado wanategemea nishati isiyo endelevu kwa ajili ya kuangazia nyumba na kupika akisema..

“ Tunahitaji kuhakikisha kuwa wana uwezo wa kupata nishati salama, na sauti ya sekta ya afya lazima iwe thabiti kushinikiza hilo na liweze kutekelezeka.”

Dkt. Maria amesema serikali nazo zilitoa mapendekezo akitoa mfano Uholanzi ambayo imeahidi kupunguza utoaji hewa chafuzi.

Image
Kwa jitihada za sasa, kufikia mwaka wa 2030 uchafuzi wa hewa utapunguzwa kwa theluthi moja tu ya viwango vinavyohitajika ili kufikia malengo. Picha: UNEP

Wengine waliahidi kuboresha mifumo ya usafiri ili kupunguza kiwango cha hewa chafuzi sambamba na kuelimisha umma juu ya uhusiano kati ya afya na hewa chafuzi.

Mkutano huo ulioanza tarehe 30 mwezi uliopita ulimalizika jana na ulileta pamoja viongozi na wakuu wa nchi, serikali, mawaziri, mameya na mashirika ya kiraia.