Baraza la Usalama lauongezea muda ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sahara Magharibi.

Askari wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko ukanda wa Sahara ya Magharibi MINURSO akiwa kazini katika eneo la Oum Dreyga ndani ya Sahara Magharibi.
UN Photo/Martine Perret
Askari wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko ukanda wa Sahara ya Magharibi MINURSO akiwa kazini katika eneo la Oum Dreyga ndani ya Sahara Magharibi.

Baraza la Usalama lauongezea muda ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sahara Magharibi.

Masuala ya UM

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jumatano hii wamepitisha azimio la kuuongezea muda wa miezi sita zaidi ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko ukanda wa Sahara ya Magharibi MINURSO huku  pia wakiunga mkono juhudi za Katibu Mkuu Antonio Guterres na mwakilishi wake maalum za kuanzisha majadiliano kabla ya mwisho wa mwaka.

Azimio hilo limepitishwa katika kikao kilichofanyika ndani ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani ambapo azimio limedhaminiwa na Marekani na kupitishwa kwa kura 12 ambapo Urusi, Ethiopia na Bolivia hawakupigaji kura.

Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Jonathan Cohen ameliambia Baraza la Usalama kuwa mambo hayawezi kuendelea kwa namna ile ile ya kawaida juu ya Sahara Magaribi.

Hivyo ametoa wito wa kumuunga mkono mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Sahara Magharibi, Horst Köhler katika juhudi zake za kutafuta suluhu inayokubalika ambayo itawapa mwelekeo thabiti watu wa Sahara Magharibi.

Hata hivyo Balozi Cohen amewatahadharisha wajumbe wenzake kuwa wasifikiri tayari wamelimaliza jambo hili kwa kuona wameufikia mstari wa mwisho wa ushindi, akisema, “ mchakato wa kisiasa ndio kwanza umeanza. Tunaamini kuwa mazungumzo ya moja kwa moja chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa yanatoa fursa ya kweli ya kufikia suluhu inayokubalika na pande zote na mkutano ujao kule Geneva, Uswisi utakuwa hatua ya kwanza ya muhimu kaatika mchakato huu. Pande zote zinatakiwa kubaki madhubuti katika mazungumzo ya mwezi disemba na kundelea mpaka mwisho wenye mafanikio”

Walinda amani wakikagua eneo baada ya amri ya kusitisha mapigano huko Smara Sahara Magharibi.
UN Photo/Martine Perret
Walinda amani wakikagua eneo baada ya amri ya kusitisha mapigano huko Smara Sahara Magharibi.

 

Mgogoro wa Sahara magharibi ulianza mwishoni wa utawala wa ukoloni wa Hispania kwenye eneo hilo mwaka 1976, ambapo mapigano yalizuka kati ya Morocco na vikundi vya Polisario. Ili Kusitisha mapigano ulisainiwa mkataba mnamo Septemba 1991.

MINURSO ilitumwa mwaka huo wa 1991 ili kufuatilia na kusimamia mkataba wa amani kati ya serikali ya Morocco na vikundi vya Polisario .

MINUSRO ilipewa jukumu la kusimamia mchakato wa kura ya maoni juu ya kujitenga kwa kwao kufuatilia makubaliano ya pande zote mbili na pia inatoa msaada kwa wahamaji ikiwa ni pamoja na kutoa misaada ya kibinadamu yanapotokea majanga ya asili.