Tuanzishe ‘ushirika wa amani’ ili kila mtu aishi kwa utu na apate fursa- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia Mkutano wa 9 wa Kimataifa wa Muungano wa Ustaarabu wa Umoja wa Mataifa huko Fez, Morocco.
UN News/Alban Mendes De Leon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia Mkutano wa 9 wa Kimataifa wa Muungano wa Ustaarabu wa Umoja wa Mataifa huko Fez, Morocco.

Tuanzishe ‘ushirika wa amani’ ili kila mtu aishi kwa utu na apate fursa- Guterres

Masuala ya UM

Katika dunia ambayo “maovu ya zamani – chuki dhidi ya wayahudi, ubaguzi dhidi ya wasio waislamu, utesaji wa wakristo, chuki dhidi ya wageni na ubaguzi – vinaendelea kupatiwa tena uhai,” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres huku akiongeza kuwa Jukwaa la Umoja wa Mataifa la Ustaarabu, UNAOC linasaidia kuonesha njia ya jinsi ya kuchukua hatua kwa mshikamano. 

Bwana Guterres amesema hayo leo huko Fez nchini Morocco wakati akihutubia mkutano wa 9 wa jukwaa hilo. 

Amesema “nguvu  ya mgawanyiko na chuki vinapata eneo jipya la kuchipua vikiimarishwa na ukosefu wa hak ina mizozo.” 

Ni kwa kuzingatia hilo, Katibu Mkuu ametoa wito wa kuundwa kwa ushirika wa amani kupitia utambuzi wa “utajiri katika utofauti,” na kuwekeza katika ujumuishi na kuhakikisha kuwa , “kila mmoja wetu bila kujali rangi yake, asili yake, jinsia, dini au hadhi, anaweza kuishi kwa utu na kupata fursa.” 

Katibu Mkuu amerejelea vitabu vitukufu akisema “Kurani Tukufu inafundisha kuwa Mungu aliumba mataifa na makabila, ‘ili tuweze kufahamiana vizuri,” huku akishi ya kwamba “katika zama za sasa za majanga, ni wakati wa kuhamasishwa na maneno kama hayo na kusimama pamoja kama familia moja ya kibinadamu yenye utajiri wa utofauti, sawa kiutu na kihaki na iliyoungana kwa mshikamano.” 

Mji wa Fez, Morocco unaandaa Mkutano wa 9 wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa Ustaarabu, ambao unafanyika chini ya kaulimbiu “Towards An Alliance of Peace: Living Together as One Humanity”.
UN News/May Yaacoub
Mji wa Fez, Morocco unaandaa Mkutano wa 9 wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa Ustaarabu, ambao unafanyika chini ya kaulimbiu “Towards An Alliance of Peace: Living Together as One Humanity”.

Moratinos: Hakuna mgongani wa ustaarabu lakini kuna mgongano wa maslahi na ukosefu wa uelewa 

Miguel Angel Moratinos, ambaye ni Mwakilishi wa Ngazi ya Juu wa Jukwaa la Umoja wa Mataifa la Ustaarabu, UNAOC akihutubia mkutano huo wa 9 wa jukwaa hilo amehoji hoja ya mwanasayansi maarufu wa siasa wa kimarekani Samuel Huntington, ametoa mhadhara wake kuhusu “Mgongano wa ustaarabu.” 

Moratinos amesisitiza kuwa, “mizozo ya kimataifa haiwezi kuwa matokeo pekee ya dini, tamaduni au ustaarabu. Kuna mgongano wa maslani na ukosefu wa uelewa.” 

Kwa mwakilishi huyo wa ngazi ya juu, dunia haikabiliwi na mgongano wa ustaarabu, kwa sababu dunia ya karne hii ya 21 imeunganika. Kwa hiyo, “sisi ni binadamu wamoja tukikabiliwa na changamoto lukuki za kimataifa.” 

“Majanga ya sasa yanakumba jamii ya kimataifa yametuonesha ya kwamba hakuna mipaka inayoweza kuzuia virusi na vita, iwe yanatokea Ulaya au kwingineko duniani,” amefafanua Moratinos akieleza kuwa “vita ya kikanda, vita nchini Ukraine imeathiri amani na utulivu duniani kote.” 

Amesema katika kutetea stahmala “hebu tutetee pia kuheshimiana, katika kutetea kuishi pamoja hebu tutetee kuishi pamoja. Katika kutetea haki za makundi madgo, hebu tutetee haki sawa kwa raia wote. Kwenye kutengana, hebu tutetee ujumuishi na udugu.” 

Azimio la Fez na msisitizo kwa wasuluhishi wanawake 

Mkutano huo wa 9 wa Muungano wa Ustaarabu umepitisha azimio la Fez linalosisitiza masuala kadhaa ikiwemo umuhimu wa elimu na wanawake kama wasuluhisji na wajenzi wa amani, halikadhalika kutokomeza ubaguzi na ukosefu wa stahmala kwa misingi ya dini au imani zozote. 

Azimio hilo pia limepongeza hatua za kimataifa ikiwemo zile za shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO za kusongesha uhifadhi wa urithi wa kitamadui wakati wa amani n ahata wakati wa mizozo, huku likisihi wadau kulaani uharibifu wa kinyume cha sheria wa maeneo ya urithi wa kitamaduni au kidini. 

Ariel Pino, mwenye umri wa miaka 12, kutoka Uhispania, mpokeaji wa tuzo ya PLURAL + Youth Video Festival.
UN Photo/May Yaacoub
Ariel Pino, mwenye umri wa miaka 12, kutoka Uhispania, mpokeaji wa tuzo ya PLURAL + Youth Video Festival.

Morocco: Washiriki wapaza sauti 

Jukwaa linafanyika wakati dunia inakabiliwa na mlolongo wa changamoto kuanzia kushamiri kwa misimamo mikali, ugaidi, chuki dhidi ya wageni, kauli za chuki na ubaguzi. 

Zaidi ya wawakilishi 1000 kutoka nchi 100 wanashiriki kwenye jukwaa hilo. 

Filamu ya “Adventure in Other Seas”, yashinda tuzo 

Katika mkutano huo ,filamu ya “Adventure in Other Seas,” au “Safari katika bahari zingine” kwa lugha ya Kiswahili ilishinda tuzo ya kushamirisha uhamiaji salama na ujumuishi. 

Tuzo hiyo imetolewa kupitia mpango wa PLURAL+ na Tamasha la video la vijana, ambao ni mpango wa pamoja wa UNAOC na shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM

Baada ya kupokea tuzo hiyo, Ariel Pino kutoka Hispani akizungumza kwa niaba ya wenzake ameshukuru kwa kutambuliwa kwa filamu hiyo. 

Filamu hiyo inahusu samaki aliyeamua kuhama jamii yake na kuelekea kwingine, machungu aliyopitia safarini lakini pia mateso kutoka kwa samaki kwenye jamii mpya. 

Ariel amesema kupitia filamu hiyo wamejifunza mambo mengi ikiwemo kujiweka kwenye mazingira ya watu wanaovuka bahari, kuchangia katika jamii mpya watu wanakohamia na zaidi ya yote kujifunza kuishi kama familia moja.