Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nina matumaini ya mustakabali bora huko Sahara Magharibi- Köhler

Kutokana na mvutano huko Sahara Magharibi, Umoja wa Mataifa ulipeleka ujumbe wake MINURSO ili kufuatilia na kusimamia mkataba wa amani kati ya serikali ya Morocco na vikundi vya Polisario .
MINURSO
Kutokana na mvutano huko Sahara Magharibi, Umoja wa Mataifa ulipeleka ujumbe wake MINURSO ili kufuatilia na kusimamia mkataba wa amani kati ya serikali ya Morocco na vikundi vya Polisario .

Nina matumaini ya mustakabali bora huko Sahara Magharibi- Köhler

Amani na Usalama

Mkutano wa siku mbili wa wawakilishi wa mkutano wenye lengo la kusaka suluhu ya mvutano kuhusu Sahara Magharibi, umemalizika huko Geneva, Uswisi kwa pande hizo kutoa tamko la pamoja ambamo wameeleta kutambua kwao kuwa ushirikiano na ujumuishaji wa kikanda ndio njia bora zaidi ya kushughulikia changamoto zinazokabili eneo lao.

Wawakilishi waliokutana kufuatia wa mwaliko kutoka kwa mjumbe binafsi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sahara Magharibi, Horst Köhler wanatoka Morocco, Polisario, Mauritania na Algeria.

Akisoma taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Bwana Köhler ambaye ni Rais wa zamani wa Ujerumani amenukuu pande hizo zikisema kuwa majadiliano yote yalifanyika katika mazingira ambamo ila pande ilishiriki kwa dhati, ukweli na kwa kuheshimiana. 

“Wajumbe wamekubaliana kuwa mjumbe binafsi atawakaribisha kwenye awamu ya pili ya mazungumzo kwenye robo ya kwanza ya mwaka ujao wa 2019.” bwana Köhler amenukuu tamko hilo la pamoja.

PANDE HUSIKA ZIMEAZIMIA KUSAKA SULUHU SAHARA MAGHARIBI

Akitoa mtazamo wake, Köhler amepongeza pande husika kwa kukutana tena baada ya miaka 6 na kurejelea azma yao ya kushiriki kwa dhati ili kusaka suluhu ya kudumu ya suala la Sahara Magharibi kwa mujibu wa azimio namba 2440 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Azimio hilo linataka suluhu halali, ya kudumu na inayokubaliwa na pande zote na ambayo itawawezesha watu wa Sahara Magharibi kujisimamia.
 
Mjumbe huyo binafsi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema “kutokana na majadiliano yetu, ni dhahiri kuwa hakuna mtu atashinda kwa kuendeleza hali ya sasa ilivyo, na ni imani yangu thabiti kuwa ni kwa maslahi ya wote kusuluhisha mzozo huu ili kuweka mazingira kwenye eneo hilo ya ukuaji thabiti wa uchumi, fursa za ajira na usalama.”

Amesema pande hizo pia zimeazimia kuendelea na mashauriano na “ni matumaini yangu kuwa mchakato huu kwanza kabisa utaongozwa na hofu inayokumba wanawake, wanaume, watoto na vijana wa Sahara Magharibi. Naamini kuna fursa ya suluhisho la amani na nasubiri kwa hamu kukaribisha tena wajumbe kwa awamu ya pili ya mazungumzo robo ya kwanza yam waka 2019.”

MZOZO WA SAHARA MAGHARIBI

Mgogoro wa Sahara magharibi ulianza mwishoni wa utawala wa ukoloni wa Hispania kwenye eneo hilo mwaka 1976, ambapo mapigano yalizuka kati ya Morocco na vikundi vya Polisario. Ili Kusitisha mapigano mkataba wa amani ulitiwa saini mnamo Septemba 1991.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko ukanda wa Sahara ya Magharibi (MINURSO) ulitumwa mwaka huo ili kufuatilia na kusimamia mkataba wa amani kati ya serikali ya Morocco na vikundi vya Polisario . MINURSO ilipewa jukumu la kusimamia mchakato wa kura ya maoni juu ya kujitenga kwa kwao kufuatilia makubaliano ya pande zote mbili.