Algeria acheni kufukuza wahamiaji na kuwatelekeza jangwani- Mtaalamu

11 Oktoba 2018

Ukatili unaokumba wahamiaji watoto na watu wazima kutoka nchi za Afrika Magharibi unapaswa kushawishi jamii yenye utu duniani kuchukua hatua, amesema mtaalamu maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

Felipe González Morales ambaye anahusika na haki za wahamiaji ametoa wito huo baada ya ziara yake nchini Niger ambako ni kituo cha wale wote wanaosaka kuelekea Ulaya kwa lengo la kupata maisha bora.

Akiwa ziarani humo amepata simulizi za kutisha ikiwemo kusafirishwa kiharamu, mateso, kukamatwa kiholela na kuswekwa korokoroni, kubakwa pamoja na watu kutumikishwa bila ajira na kushikiliwa utumwani.

“Wahamiaji hawa katika safari za kuelekea Niger, wanapitishwa Sudan, Chad na Mali,” amesema Bwana Gonzales ambapo licha ya kupongeza Niger kwa ukarimu wake amezungumzia sheria mpya za uhamiaji ambazo zimegeuza nchi hiyo kuwa lango la kusini la kuingilia barani Ulaya.

Amegusia pia jinsi sheria yam waka 2015 ya kudhibiti usafirishaji haramu wa wahamiaji ambayo imesababisha kuwepo kwa tabia ya kuzuia wahamiaji kuelekea kaskazini mwa Niger na hivyo kuchochea wahamiaji kutumia njia za hatari zaidi.

Bwana Gonzales amesisitiza kuwa sera za uhamiaji hazipaswi kujikita tu katika kigezo cha usalama bali pia haki za binadamu zinapaswa kuwa msingi wake.

Amesema msaada wowote wa kimataifa na Muungano wa Ulaya unapaswa kusaidia taifa hilo kuangalia upya mkakati wake wa uhamiaji.

Mtaalamu huyo maalum wa uhamiaji pia ameangazia Algeria akiitaka isitishe mpango wake wa kuwafukuza wahamiaji kutoka Niger na mataifa mengine ya Afrika Magharibi.

Yaelezwa kuwa hadi sasa Algeria imefukuza wahamiaji 17,000 mwaka huu pekee jambo ambalo limekanushwa na nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

 Mtaalamu huyo amesema “nimesikia shuhuda kutoka kwa wahamiaji wanawake, wanaume na watoto ambao walivamiwa kwenye nyumba zao usiku wa manane na kukamatwa kiholela, walipigwa na hatimaye kusafirishwa kwenye lori  umbali wa kilometa 15 kutoka mpaka wa Algeria na Niger na hatimaye kutelekezwa.”

Habari hizi za wahamiaji kukumbwa na zahma zinakuja wakati huu ambapo jamii ya kimataifa inaendelea na jitihada zake za kusaka suluhu kupitia mkataba wa uhamiaji salama na wa kihalali, Global Compact for safe, orderly and regular migration.

Mkataba huo unatarajiwa kupitishwa huko Marrakesh Morocco baadaye mwaka huu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud