Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhamiaji uwe ajenda ya kisiasa barani Afrika

Wahamiaji hawa wakihesabiwa kabla ya kusafirisha kwa boti kutoka Obock, kaskazini mwa Djibouti kuelekea Yemen. Licha ya mzozo Yemen bado watu wanamiminika kusaka hifadhi.
Kristy Siegfried/IRIN
Wahamiaji hawa wakihesabiwa kabla ya kusafirisha kwa boti kutoka Obock, kaskazini mwa Djibouti kuelekea Yemen. Licha ya mzozo Yemen bado watu wanamiminika kusaka hifadhi.

Uhamiaji uwe ajenda ya kisiasa barani Afrika

Wahamiaji na Wakimbizi

Mkutano wa siku mbili kuhusu uhamiaji barani Afrika umekunja jamvi huko Geneva, Uswisi ambapo washiriki wametaka viongozi wa bara hilo wahamasishwe ili uhamiaji iwe ajenda ya kisiasa kwa nchi zao.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mtendaji wa kamisheni ya uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa nchi za Afrika, ECA, Bi, Vera Songwe amesema ni vyema kuwaeleza viongozi hao kuwa uhamiaji katu haukandamizi demokrasia na utawala bora.

Kwa mantiki hiyo amesema wanshirikiana na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM ili kuweza kuweka dhahiri manufaa ya uhamiaji kwa bara la Afrika.

Naye Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleag akihutubia kikao hicho amesema tatizo ni kwamba “tumeruhusu fikra potofu kuhusu uhamiaji zienee kuliko kweli halisi. Badala ya kuangalia kwa kina manufaa ya uhamiaji na kuweka kwenye sera zetu.”

Ametaka matokeo ya kikao hicho yatumike kuchagiza kwa dhati zaidi ukusanyaji wa michango ya wahamiaji kwenye ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu.

Mkurugenzi Mkuu wa IOM, William Lacy Swing, akaweka bayana kuwa watu bilioni moja hivi sasa kote ulimwenguni wanahama kutoka eneo moja kwenda lingine. “Kiwango hiki ni zaidi ya wakati wowote katika historia ya dunia,” amesema Swing akiongeza kuwa mtazamo  hasi kuhusu janga la uhamiaji ni sawa na kimbunga.

Amesema baadhi ya nchi zinaendelea kutetea uhalisia ambao hauko tena hivi sasa na kutaka watu watambue michango ya kihistoria iliyoletwa na wahamiaji katika maeneo mbalimbali duniani.

Mkutano huo umelenga kuandaa mapendekezo ya kujenga hoja ya Afrika ya kutaka kuwepo kwa uhamiaji salama na wenye mpangilio na hivyo kuchangia katika makubaliano ya kimataifa ya uhamiaji, GCM.

IOM, ECA, GCM, Uhamiaji