Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nahisi nawajibika na kifo cha kila mlinda amani- Guterres

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania walio kwenye kikosi maalum cha kujibu mashambulizi cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC.
MONUSCO Forces/FIB-TANZBATT
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania walio kwenye kikosi maalum cha kujibu mashambulizi cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC.

Nahisi nawajibika na kifo cha kila mlinda amani- Guterres

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa na nchi zinazochangia kwenye operesheni za ulinzi wa amani wa chombo hicho leo wamekuwa na kikao cha ngazi ya juu kuangazia jinsi ya kuimarisha operesheni hizo.

Mkutano huo ulianza kwa video mahsusi ya kuonyesha mafanikio ya operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa ambazo mwaka huu zimetimiza miaka 70.

Kisha Katibu Mkuu Antonio Guterres akaanza hotuba yake kwa kuelezea uzoefu wake wa machungu alipoweka shada la maua huko Jamhuri ya Afrika ya Kati kufuatia vifo vya walinda amani wawili.

Katibu Mkuu akasema anahisi anawajibika na kifo cha kila mlinda amani na kwamba “wengi wenu ndani  ya ukumbi huu nanyi mmepitia uzoefu huu.”

Na ndipo Katibu Mkuu akaomba wajumbe wasimame kwa dakika moja ili kukumbuka walinda amani waliopoteza maisha wakiwa kwenye huduma ya hiyo.

A4P INALENGA NINI?

Idadi ya ofisi za  Umoja wa Mataifa zinazohusika na ulinzi wa amani
UNPeacekeeping
Idadi ya ofisi za Umoja wa Mataifa zinazohusika na ulinzi wa amani

Guterres akasema ni kwa kuzingatia changamoto za ulinzi wa amani ikiwemo mauaij ya walinda amani, ndio maana ameanzisha mkakati wake wa hatua za pamoja kwa ajili ya ulinzi wa amani, A4P mwezi Machi mwaka huu.

Amesema A4P inalenga kuimarisha matarajio makuu mawili ya msingi katika operesheni za ulinzi wa amani akisema mosi,  “tunapaswa kuchukua hatua zaidi kusongesha suluhu za kisiasa. Walinda amani wanapelekwa kuandaa mazingira bora ya wao wenyewe kuondoka; na ndio maana kuna uhusiano kati ya ujumbe wa ulinzi wa amani na nchi mwenyeji.”

Guterres amesema ulinzi wa raia nao ni hoja ya pili na ni jukumu muhimu kwa walinda amani. “Katu hatuwezi kusahau matokeo ya kutisha yaliyotokana na kushindwa kwetu.”

Katibu Mkuu amesema ubia na mashirika ya kikanda ni muhimu katika kufanikisha malengo ya kisiasa na ya kiutendaji akitolea mfano jinsi Muungano wa Afrika umekuwa na msaada mkubwa wakati wa harakati za kukabiliana na uagidi au kuimarisha amani.

ULINZI WA AMANI NI ZAIDI YA KULINDA AMANI

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na marais, wakuu wa nchi na mawaziri, Guterres ameenda mbali akisema kuwa mafanikio ya ulinzi wa amani ni zaidi ya kulinda amani.

Walinda amani wanalinda mamilioni ya wakimbizi wa ndani na kusaidia ufikishaji wa misaada ya kibinadamu ya kuokoa maisha.  “Nimeshuhudia kwa macho yangu, nimetembelea Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Uganda ambako nimekutana na wakimbizi kutoka Sudan Kusini. Nimezungumza na watu ambao wanasema uhai wao unatokana na walinda amani wa Umoja wa Mataifa.”

Wakati wa harakati za mazoezi ya kuokoa wagonjwa, helikopta ikipaa kutoka eneo la Gao nchini Mali huku walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Canada wakijikinga na vumbi
MINUSMA/Marco Domino
Wakati wa harakati za mazoezi ya kuokoa wagonjwa, helikopta ikipaa kutoka eneo la Gao nchini Mali huku walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Canada wakijikinga na vumbi

Kwa upande wake Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema katika hali ya kawaida, walinda amani hawahitajiki lakini kwa sababu ya mazingira yalivyo hakuna jinsi. Hata hivyo amesisitiza suala la ushirikiano wa kikanda, lakini akitaka usaidizi wa kifedha pindi unapotakiwa au unapokuwa umeahidiwa utekelezwe ili walinda amani waweze kufanya kazi yao.

Waziri Mkuu wa Bangladesh, Sheikh Khasina ambaye naye nchi yake inachangia walinda amani kwa Umoja wa Mataifa amezungumzia jinsi walivyoitikia wito wa kuongeza walinda amani wanawake kwenye vikosi vyake akisema tayari wamepelekwa huko Jamburi ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.