Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAM kusaidia kuepusha njaa duniani

Wanawake huko Ganyiel jimbo la Unity nchini Sudan Kusini wakisubiri mgao wa chakula. Hali ni mbaya ya chakula.
OCHA/Gemma Connell
Wanawake huko Ganyiel jimbo la Unity nchini Sudan Kusini wakisubiri mgao wa chakula. Hali ni mbaya ya chakula.

FAM kusaidia kuepusha njaa duniani

Msaada wa Kibinadamu

Bila kumaliza njaa hatuwezi kwenda popote na kuridhika na maendeleo yetu kuhusu ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, wakati wa kuzindua mpango tekelezi dhidi ya njaa, FAM mjini New York Marekani leo Jumapili.
 
Amesema kuwa azma ya kuwa na ulimwengu usiokumbwa na njaa ni lengo muhimu ambalo linafaa kushughulikiwa akieleza kuwa wakati huu wa maarifa tele  kuhusu kilimo pamoja na teknolojia, bila shaka, “ tunaweza kuhakikisha haki ya kila mtu ya kupata chakula,”amesema.

Ukame  unazidi kuathiri ardhi ya sehemu kubwa katika  bara la Afrika.
UNICEF/Mukwazhi
Ukame unazidi kuathiri ardhi ya sehemu kubwa katika bara la Afrika.


 
Ameongeza kuwa la kusikitisha ni kuwa bado kuna picha za wazazi wakiwa wamebeba watoto waliokondeana kutokana  na utapiamlo, wakiwa hawajui la kufanya kutokana na hali hiyo.
 
Amesema kuwa  mwaka jana watu zaidi ya milioni 20, katika eneo la kaskazini mashariki mwa  Nigeria, Somalia, Sudan Kusini na Yemen, walikabiliwa na njaa.
Amesema katika eneo moja la Sudan Kusini ukame ulisababisha njaa kwa watu wengi.
Hata hivyo amesema waliweza kubadili hali kwa kuchukua hatua za haraka hususan katika mataifa manne.
 
 Amesema kuwa baada ya miaka kadhaa ya maendeleo ya *kuondokana na njaa yaonekana kama jamii ya kimataifa inashindwa *kwani idadi ya wasiokuwa na chakula cha kutosha inazidi kupanda  hadi zaidi ya milioni 820  katika mwaka wa 2017.
 
Katibu Mkuu amesema kuwa katika dunia hii yenye vitu vingi lakini mtu mmoja kwa kila watu tisa  *hana* chakula chakutosha na takriban watoto milioni 15 hawapati chakula cha kutosha  na wanakaribia kudumaa katika maisha yao yote.
 
Anasema licha ya hali hiyo kuna sababu nyingi za kuweza kubadili mkondo huo, kama vile migogoro inayosambaa, kuongezeka kwa kutokuwa na usawa pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.
 
Amesema kuwa jibu lao kuhusu ongezeko hilo la mgogoro wa njaa ni lazima liwe na mwelekeo wa aina kadhaa , kutoka uzuiaji, hatua ya kibinadamu pamoja na maendeleo endelevu.
 

Mama na mtoto wake katika sehemu za Ethiopia ambako majanga ya asili kama vile ukame na mafuriko yanawasumbua tena ongeza mapigano kati ya makabila.
OCHA/Charlotte Cans
Mama na mtoto wake katika sehemu za Ethiopia ambako majanga ya asili kama vile ukame na mafuriko yanawasumbua tena ongeza mapigano kati ya makabila.


Bwana Guterres amesema kuwa mpango tekelezi kuhusu njaa -FAM- ni chombo kipya ambacho kitasaidia kutabiri na hivyo kuweza kuzuia kuondoa shida ya chakula na ukame kabla havijatokea.
 
 Ameongeza kuwa , kwa mara ya kwanza, FAM itatumia teknolojia ya kisasa ikiwemo mashine ambazo zinatambua uhusiano katika hali tofauti.
Ametoa shukrani kwa washirika wao Amazon, Google na Microsoft kwa usaidizi wa kuunda vyombo hivyo.
Amerejelea azma yao ya kumlisha kila mtu duniani na kutomuacha  yeyote nyuma.