Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu yasalia ndoto kwa watoto milioni 303 duniani- Ripoti

Watoto wako darasani wakisoma.
UNICEF/Loulou d’Aki
Watoto wako darasani wakisoma.

Elimu yasalia ndoto kwa watoto milioni 303 duniani- Ripoti

Utamaduni na Elimu

Watoto  na barubaru milioni 303 duniani kote hawako shuleni na hivyo kutishia mustakhbali wa kundi hilo lenye umri wa kati ya miaka 5 hadi 17, imesema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

Ikipatiwa jina la mustakhbali uliopokwa-ni kijana lakini hayuko shuleni,ripoti inaangazia zaidi nchi zenye mizozo ikisema watoto na barubaru milioni 104 kati yao wako katika nchi zilizogubikwa na mizozo.

Ripoti inabainisha kuwa katika nchi hizo zenye majanga, mtoto 1 kati ya 5 mwenye umri wa kati ya miaka 5 hadi 17 hajawahi kuingia darasani, huku 2 kati ya watano hawakumaliza  shule ya msingi.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore, akigusia ripoti hiyo amesema kuwa taifa linapokumbwa na mgogoro au majanga, madhara yake kwa watoto na barubaru huwa maradufu.

Amesema shule zao zinaharibiwa, hukaliwa na vikosi vya jeshi, au hushambuliwa makusudi na huwa sehemu ya mamilioni ya watoto ambao hawasomi na kwamba kadri muda unavyosonga hawarejei tena shuleni.

Bi. Fore amesema wakati huu ambapo maombi ya fedha kwa ajili ya elimu ni asilimia 4 pekee ya maombi ya fedha za misaada ya kibinadamu duniani, ni vyema kuwekeza zaidi kwenye elimu bora hususan katika maeneo yenye mizozo, ili watoto na vijana waweze  kusoma katika mazingira salama.

Anasema hatua hiyo itakuwa ni uwekezaji bora kwa kuwa ifikapo mwaka 2030 idadi ya watoto na barubaru wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 19 itaongezeka na kufikia zaidi ya bilioni1.3, hivyo kuwapatia stadi bora ni mbinu sahihi ya kuwawezesha kuchangia kwenye maendeleo endelevu.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa kabla ya kuanza mwa mjadala wa ngazi ya juu wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imeangazia hali ya elimu kwa watoto na vijana  kuanzia shule za chekechea hadi sekondaria katika mataifa mbalimbali yakiwemo yaliyoathiriwa na dharura za kibinadamu.