Maendeleo yanayotokomeza urithi wa binadamu si maendeleo

19 Septemba 2018

Msingi wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ni utambuzi ya kwamba maendeleo yasiyotambua watu kama wanufaika wakuu wa hatua hiyo si maendeleo bali uchumi usio na manufaa.

Naibu Kamishna Mkuu wa tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Kate Gilmore, amesema hayo leo mjini Geneva, Uswisi kwenye mjadala wa kila mwaka wa Baraza la haki za biandamu, kuhusu haki za watu wa asili katika maendeleo na utekelezaji wa ajenda 2030.

Bi. Gilmore amesema SDGs imetambua kuwa maendeleo ambayo yanaharibu tamaduni, lugha, ardhi na urithi wa binadamu si maendeleo bali ni uharibifu wa makusudi.

Amesema suala la maendeleo yasiyojali binadamu limekuwa dhahiri zaidi kwa ulimwengu wa watu wa jamii za asili akisema wakati jamii hizo katu hazikuweza kunufaika na maendeleo ya dunia na badala yake zimekuwa waathirika hasi wa maendeleo.

Wamasai kutoka Kenya
UN /Andi Gitow
Wamasai kutoka Kenya

 

Ameeleza kuwa “watu  milioni 370 wa jamii za asili ambao wametapakaa katika mataifa 70 ndiyo mfano bora wa watu ambao wamebaguliwa  na pia kubaki nyuma kimaendeleo kuliko wote. Hii ina maana kwamba ajenda ya mwaka 2030 haitatimizwa  ikiwa jamii ya kimataifa haitatekeleza  haki za watu wa asili.

Nao washiriki wengine wamekubali kuwa  watu  wa asili wanaendelea kubaguliwa na kutilia mkazo  umuhimu wa kuwashirikisha watu hao katika juhudi za kimaendeleo.

Pia wamekumbusha kuwa  mapendekezo 999 ya mapitio ya kila mwaka ya nchi kuhusu haki za binadamu hayakujumuisha masuala ya uzoefu na changamoto wanazokabiliana nazo watu wa asili pamoja na ukiukwaji wa haki zao wale wanaofanya mapenzi ya jinsia moja na waliobadili jinsia.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter