Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limeonya kuwa visa vya ugonjwa wa surua vinaongezeka kwa kiwango kikubwa duniani nchi 10 zikiongoza kwa zaidi ya asilimia 74 ya jumla ya ongezeko na pia nchi nyingine zikiwa zile ambazo awali zilikuwa zimeshatangazwa kuutokomeza kabisa ugonjwa huo.
Kwa mujibu taarifa ya UNICEF iliyotolewa jijini New York, Marekani siku ya Alhamisi, nchi zipatazo 98 duniani kote zililiripoti maambukizi mengi zaidi ya surua kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na mwaka 2017, jambo ambalo linarudisha nyuma hatua zilizokwishapigwa dhidi ya ugonjwa huu unaozuilika lakini wa hatari.
Ukraine, Ufilipino na Brazil zimetajwa kushuhudia ongezeko kubwa la maambukizi ya surua kutoka mwaka 2017 hadi 2018.
Huko Ukraine pekee kulikuwa na wagonjwa 5,120 wa surua kwa mwaka 2018 huku watu wengine 24,042 wakiripotiwa kuugua Surua miezi miwili ya mwaka huu wa 2019.
Nchini Ufilipino mwaka huu pekee kumeripotiwa visa 12,736 vya surua na vifo 203 ikilinganishwa na maambukizi kwa watu 15,599 katika mwaka mzima wa 2018.
Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta H.Fore amesema, “hii ni tahadhari ya kutuamsha. Tuna chanjo dhidi ya ugonjwa huu wa kuambukiza ambayo ni salama na inayofaa tena si ya gharama, chanjo ambayo imewaokoa takribni watu milioni moja kila mwaka kwa kipindi cha miongo miwili.”
Amesema “maambukizi haya hayajatokea kwa usiku mmoja tu.Kama tunavyoona mlipuko hatari tunaouona hivi sasa ulianza tangu mwaka jana 2018, kutokuchukua hatua leo kutakuwa na athari mbaya kwa watoto kesho.”
Katika kupambana na milipuko ya surua, UNICEF na wadau wake wanazisaidia serikali za nchi mbalimbali kuwafikia watoto kote ulimwenguni kama vile Ukraine, Ufilipino, Brazili, Yemen, Madagascar na kwingineko.
Surua ni ugonjwa wa kuambukiza zaidi kuliko hata Ebola, Kifua kikuu au mafua. Hata baada ya saa mbili baada ya mgonjwa kuondoka katika chumba, virusi vya suruu vinaweza kumwambukiza mtu mwingine atakayeingia.