Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mipango miji ni chachu ya maendeleo endelevu:FOS4G 2018

Picha kutoka akaunti ya Twitter ya UNHCR Kenya.
Mkimbizi akichora sanaa baada ya warsha iliyoendeshwa na Victor Ndula na Shirika la FilmAid International.

Mipango miji ni chachu ya maendeleo endelevu:FOS4G 2018

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Miji endelevu iliyochagizwa namipango miji ni moja ya vichocheo vya maendeleo endelevu au SDG limesema jukwaa la kimataifa la FOSS4G lililokunja jamvi jumatatu nchini Tanzania, likitoa wito wa kutumia kila binu kuhakikisha lengo la miji endelevu kwa kutumia teknolojia linatimia. 

Ingawa wasanii wa uchoraji wanaweza wasiwe na utaalam wa mipango miji, mawazo yao yanaweza kusaidia kuipanga miji kwa kiasi cha kuwa miji stahamala. Hiyo ni Imani aliyonayo kijana Ismail Biro wa Tanzania Bora Initiative mmoja wa walioshiriki mkutano  huo, uliowaleta pamoja wadau zaidi ya 1000 kutoka nchi mbalimbali duniani ukiwemo Umoja wa Mataifa. 

Japo wengi waliokutana ni wataalamu wa ramani za kupanga miji, kijana Ismail Biro ameshiriki akiwa na wazo tofauti kiasi, akizungumza na Stella Vuzo afisa habari wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa , UNIC jijini Dar es Salaam amesema anaamini kuwa wasanii wanaweza kuchangia katika mipango miji.

“Muda mwingi watalaam ambao wapo kwenye ramani au watalaam ambao wako kwenye mipango miji ndiyo peke yao inabidi wakae na kufanya hizi shughuli, lakini kwa namna ya pekee kabisa kupitia Benki ya Dunia wakaona kwamba kuna haja ya kuwaleta wasanii kama wale ambao wanachora michoro na kuangalia kwamba kwa Sanaa ambayo wanaitumia mji stahamala una picha gani. Kwa hiyo tukaweza kuwashirikisha wasanii 35 ambapo tukaweza kupata mshindi ambaye kwa namna kubwa alikuwa anaangalia ni kwa namna gani Dar salaam inaweza kuwa ya kijani na stahamala ili kupambana na mafuriko na dhoruba nyingine”

Ismail anaamini penye wengi hakiharibiki kitu na malengo yanaweza kutimia.

“Wananchi, taasisi zisizo za kiserikali, mashirika ya maendeleo, serikali yenyewe, wakija pamoja wakaweza kutoa elimu lakini pia wakashirikiana katika kuboresha hii miundombinu ndipo unaweza kupata mji ambao umeendelea na mji ambao hauko katika hatari ya kukumbwa na matatizo”

Mawazo ya Ismail na wataalam wengine huenda yakawa dawa mujarabu ya tatizo la kanzi data linaloelewa na waandaji wa mkutano kuwa kubwa barani Afrika na duniani kote.

Mkutano huo uliokamilika jumatatu, umeandaliwa na FOSS4G, Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa na wadau wengine na umetoa fursa kwa washiriki kubadilishana mawazo kuhusu umuhimu na faida ya kutumia teknolojia kuleta maendeleo na kuboresha kanzi data.