Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Annan afananishwa na dira ya bora zaidi ya maadili

Mwendazake aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, KofI Anna pamoja na Umoja wa Mataifa walitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel 2001.
UM Picha/Sergey Bermeniev
Mwendazake aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, KofI Anna pamoja na Umoja wa Mataifa walitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel 2001.

Annan afananishwa na dira ya bora zaidi ya maadili

Masuala ya UM

Kufuatia  kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Saba wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa pamoja na watu waliowahi kufanya naye kazi wameendelea kutoa salamu zao za rambirambi kwa kiongozi huyo aliyeelezwa kuwa ni bingwa wa utu wa kibinadamu.

Mwendazake Kofi Annan, Katibu Mkuu wa Saba wa Umoja wa Mataifa, hapa alikuwa akipokea tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2001,  akisema amani lazima isakwe kuliko kitu chochote kwa sababu ni kigezo muhimu ili kila binadamu aweze kuishi  maisha yenye utu na salama.

Ni Katibu Mkuu wa kwanza kutoka miongoni mwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na amefariki dunia Jumamosi asubuhi huko Uswisi.

Kifo chake kimeshtua wengi ambapo hii leo huko mjini Mogadishu Somalia, ofisi za Umoja wa Mataifa za usaidizi kwa nchi hiyo UNSOM zimekuwa na tukio maalum la kumkumbuka.

Bendera ya Umoja wa Mataifa ikipepea nusu mlingoti, Peter de Clercq  ambaye ni Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo amesema dunia imepoteza bingwa wa amani, utu wa kibinadamu na zaidi ya yote dira kubwa ya  maadili.

Huko Nepal, wafanyakazi wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP nao walinyamaza kwa dakika moja kumkumbuka na kusema kuwa alikuwa shinikizo thabiti la mambo mema duniani.

Nchini Afghanistan, kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa, UNAMA, wafanyakazi wamemkumbuka mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel alivyotembelea Kabul mwaka 2002 na ujumbe wa kusaidia watu waliokata tamaa.

Na katika ofisi za Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi, wafanyakazi wamesema atakumbukwa kwa jinsi alivyofanyia marekebisho chombo hicho ili kiweze kuwa na msaada zaidi kule ambako kilihitajika.