Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Annan kuzikwa leo Accra, Guterres kushiriki

Mwendazake Kofi Annan, hapa ni wakati alipokuwa Katibu Mkuu wa UN akifungua kikao cha malengo ya milenia kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka 2000
UN/Eskinder Debebe
Mwendazake Kofi Annan, hapa ni wakati alipokuwa Katibu Mkuu wa UN akifungua kikao cha malengo ya milenia kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka 2000

Annan kuzikwa leo Accra, Guterres kushiriki

Masuala ya UM

Macho na masikio leo yanaelekezwa huko Accra Ghana kwenye mazishi ya mwanadiplomasia nguli na Katibu Mkuu wa 7 wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan aliyefariki dunia mwezi uliopita.

Katika mji mkuu wa Ghana, Accra hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anaungana na maelfu ya waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa 7 wa umoja huo.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa mwendazake Annan atazikwa katika makaburi ya kijeshi  yaliyopo kwenye kambi ya Burma, eneo la makao makuu ya jeshi la Ghana.

Mwili wa Annan uliwasili Accra tarehe 10 mwezi huu wa Septemba ukiambatana na mkewe, wanae pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

Raia huyo wa Ghana ambaye alishinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2001 akiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, aliteuliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 13 mwezi disemba mwaka 1996 kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na hatimaye kuidhinishwa na Baraza Kuu na kisha kuanza kutekeleza jukumu hilo tarehe 1 Januari mwaka 1997.

Annan ambaye alizaliwa tarehe 8 mwezi Aprili mwaka 1938 alifariki dunia tarehe 18 mwezi uliopita huko Berne nchini Uswisi baada ya kuugua kwa muda mfupi na ameacha mke na watoto watatu.