Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hukumu ya Monsanto ni ushindi kwa haki za binadamu

Dawa za kuulia wadudu wanaoshambulia mazao zinapaswa kuwekewa maelezo ya kutosha ili zisiwe na madhara kwa watumiaji
UNDP Uganda/Luke McPake
Dawa za kuulia wadudu wanaoshambulia mazao zinapaswa kuwekewa maelezo ya kutosha ili zisiwe na madhara kwa watumiaji

Hukumu ya Monsanto ni ushindi kwa haki za binadamu

Haki za binadamu

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamekaribisha uamuzi wa mahakama huko California nchini Marekani wa ya kutaka malipo ya fidia ya dola milioni 289 kwa mtu ambaye alipata saratani baada ya kuwa karibu na dawa ya kuulia magugu.

Mtu huyo Dewayne Johnson alikuwa mtumishi wa bustani kwenye shule moja ambapo aliieleza mahakama kuwa kampuni hiyo ya Monsanto haikuweka onyo kwenye dawa hiyo ya kwamba inaweza kusababisha saratani.

Mahakama iliridhia tarehe 10 mwezi huu na hivyo na kuagiza Monsato illipe dola milioni 39 ya fidia, dola milioni 250 kama adhabu.

Uamuzi huo wa mahakama unaakisi tathmini yam waka 2015 ya shirika la afya ulimwenguni, WHO ya kwamba Glyphosate ambacho ni kiambato kikuu cha dawa ya magugu itengenezwayo na Monsanto, inaweza kusababisha saratani kwa binadamu.

Kupitia taarifa yao iliyotolewa Geneva, Uswisi hii leo, wataalamu hao wamesema uamuzi huu ni kielelezo cha utambuzi wa haki za binadamu na wajibu wa kampuni ambapo Monsanto ilipaswa kueleza watumiaji kuhusu hatari za dawa hiyo kusababisha saratani.

Hilal Elver, Mtaalamu maalum wa UN kuhusu haki ya chakula
UN / Evan Schneider
Hilal Elver, Mtaalamu maalum wa UN kuhusu haki ya chakula

Mmoja wa wataalamu hao Hilal Elver ambaye amejikita kwenye haki za chakula, amesema matumizi yasiyo salama ya dawa, au matumizi ya kupita kiasi yana madhara mapana kwa haki za binadamu ikiwem haki ya kuishi, chakula, maji, afya pamoja na mazingira salama.

Kwa mujibu wa uamuzi huo wa mahakama, nyaraka za ndani za kampuni hiyo zinaonyesha kuwa Monsanto ilitambua kwa miongo kadhaa kuwa Glyphosate na Roundup zinaweza kusababisha saratani.

Taarifa ya wataalamu hao inasema kuwa Bwana Johnson ambaye ni mlalamika anaugua saratani na madaktari wamemweleza kuwa hatoweza kuishi zaidi ya mwaka 2020.

“Tunasikitika kuwa uamuzi huu umechelewa sana kwa kuwa Bwana Johnson anaugua saratani hatua ya mwisho. Hakuna fidia yoyote ya fedha ambayo inaligana na uhai. Tunatuma salamu zetu za pole kwa machungu anayopitia na tunampongeza kwa ujasiri wake na utashi usiotikisika wa kusaka haki zake,” wamesema wataalamu hao.

Wataalamu hao wamehitimisha taarifa yao wakisema kuwa “uamuzi huu ingawa unakatiwa rufaa ni onyo thabiti kwa kampuni za kemikali na wafanyabiashara ya sekta ya  kilimo kuepuka matumizi ya dawa kali au kuweka maonyo ya mapema na kuzingatia haki za binadamu badala ya faida.”

Uamuzi huu umetolewa ikiwa ni wiki chache kabla Bi. Elver hajawasilisha mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani ripoti yake kuhusu haki za wafanyakazi wa mashambani.