Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujira mdogo katika sekta ya uvuvi ni mtihani kwa wafanyakazi na familia zao:Mtaalam

Boti nyingi za uvuvi haramu huendesha shughuli zao kwenye maeneo ambako si rahisi kufuatiliwa lakini ndege zisizo na rubani huweza kufika.
IFAD/Franco Mattioli
Boti nyingi za uvuvi haramu huendesha shughuli zao kwenye maeneo ambako si rahisi kufuatiliwa lakini ndege zisizo na rubani huweza kufika.

Ujira mdogo katika sekta ya uvuvi ni mtihani kwa wafanyakazi na familia zao:Mtaalam

Haki za binadamu

Mishahara midogo, mazingira duni ya kazi kwa katika vyombo vya  uvuvi, ufugaji wa samaki na miundo mbinu mibovu ya viwanda vya usindikaji ni vina athari kubwa katika maisha ya kila siku ya wafanyakazi. 

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya chakula, Hilal Ever amesema hayo mjini Geneva, Uswisi hii leo wakati akiwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo.

Amesema idadi kubwa ya wafanyakazi milioni 120 wanaofanya kazi kwenye sekta ya uvuvi, mara nyingi hufanya kazi katika mazingira magumu na wakati mwingine hadi saa 20 kwa siku na hata ujira wanaopata hautoshelezi mahitaji muhimu ya familia.

Ujira wanaopata wafanyakazi milioni 5.7 kati ya hao ni chini  ya dola moja kwa siku kiasi kwamba hautoshelezi kukidhi mahitaji muhimu ya familia kama vile chakula, malazi, makazi, elimu na huduma ya afya.

Bi. Ever amesema chanzo kikubwa cha ujira mdogo ni ongezeko la mahitaji ya samaki kwa bei nafuu, samaki aina ya jodari, samoni na kamba.

Amesema wanawake na watoto nao hawaonekani dhahiri kwenye sekta hiyo, lakini ukweli ni kwamba wanatumikishwa kwenye viwanda vya kuchakata samaki ikiwemo kuchuna kamba walioganda kwenye barafu kwa saa kadhaa bila ya vifaa vya kujikinga.

Watoto nao wanatumikishwa kwa ujira mdogo kwenye boti za uvuvi bila kujali mazingira hatarishi kwa maisha yao.

Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa serikali kuzingatia wajibu wao wa kisheria wa kuheshimu na kulinda haki za wafanyakazi katika sekta ya uvuvi huku pia akitaka walaji wa samaki kusaidia kuboresha mazingira ya kazi ya wafanyakazi hao kwa kununua samaki waliovuliwa kwenye maeneo yao na wavuvi wadogo.

TAGS: Sekta ya uvuvi, samaki, Hilal Ever