Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kinachotokea Gaza kinaweza kuwa uhalifu wa kivita- Bachelet 

Michele Bachelet , Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari 26 Septemba kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York (Maktaba)
Picha na UN/Laura Jarriel
Michele Bachelet , Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari 26 Septemba kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York (Maktaba)

Kinachotokea Gaza kinaweza kuwa uhalifu wa kivita- Bachelet 

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amezitaka pande zote kwenye mapigano huko Ukanda wa Gaza ziheshimu sheria za kimataifa na pia zichukue hatua kuacha mapigano ambayo yanazidi kufanya hali kuwa mbayá nchini Israel na maeneo yanayokaliwa ya wapalestina.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi, Bi. Bachelet amesema katika siku 10 zilizopita, hali katika maeneo hayo imekuwa inatisha.  

Amesema, “hali katika eneo la Sheikh Jarrah huko Yerusalem Mashariki iliyochochea na vitisho vya kufurushwa kwa familia za kipalestina, uwepo wa wanajeshi wa Israel na ghasia katika msikiti wa Al Aqsa wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na kuendelea kwa mashambulizi kutoka na kuelekea Gaza  vimesababisha mashambulizi na idadi ya wahanga upande wa maeneo yanayokaliwa ya wapalestina na Israel.” 

Kamishna huyo Mkuu amesema viongozi wa pande zote mbili badala ya kusaka mbinu za kumaliza mvutano, wanashindana kutoa kauli za uchochezi wakati huu ambapo idadi ya watu wanaopoteza maisha na kujeruhiwa inazidi kuongezeka na wengine wakilazimika kukimbia makwao “katika kile ambacho kinaweza kusababisha ukiukwaji mkubwa wa sheria za haki za kibinadamu.” 

Bi. Bachelet ameonya kuwa urushaji wa makombora kiholela unaofanyw ana makundi ya wapalestina wenye silaha kuelekea Israel ikiwemo maeneo yenye watu wengi, ni ukiukwaji dhahiri wa sheria za kimataifa za kibinadamu na unaweza kuwa uhalifu wa kivita. 

“Huko Gaza nako vikosi vya Israel vinarusha mashambulizi kutoka angani, ardhini na baharini kuelekea maeneo yenye makazi ya watu wengi na kuna wasiwasi kubwa baadhi ya makombora kutoka Israel yanalenga maeneo ya raia ambayo kwa mujibu wa sheria siyo maeneo ya kijeshi yanayopaswa kulengwa,”  amesema Bi. Bachelet. 

Ametoa wito kwa pande zote kuheshimua sheria na wajibu wao chini ya sheria za kimataifa na kwamba, “Israel ambayo inakalia maeneo ya Palestina ina wajibu wa kuhakikisha kuwa hakuna vikwazo vyovyote vya kufikisha misaada ya kibinadamu kwenye ukanda wa Gaza.” 

Bi. Bachelet amteoa wito pia kwa serikali ya Israel kuchukua hatua kudhibiti kusambaa kwa ghasia kati ya vikundi vyenye misimamo mikali ikiwemo miongoni mwa walowezi wa kiyahudi, raia wa kipalestina huko Israel kwenye miji ya Lod, Jaffa, Ramle na Haifa.