Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hamas waishambulia Israel karibu na Ukanda wa Gaza, viongozi UN wahamasisha amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (Picha ya maktaba)
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (Picha ya maktaba)

Hamas waishambulia Israel karibu na Ukanda wa Gaza, viongozi UN wahamasisha amani

Amani na Usalama

Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa wametuma ujumbe kwa pande zote zinazohusika na mzozo wa Palestina na Israel ili kuwahimiza “kujizuia zaidi" kufuatia "matukio ya kutisha ya vurugu" ambayo yamesababisha vifo vya watu kadhaa na mamia kujeruhiwa katika miji ya Israel karibu na Ukanda wa Gaza huku kukiwa na mashambulizi ya roketi ya wanamgambo wa Kipalestina wenye silaha mapema Jumamosi asubuhi.

 

 

Katibu Mkuu UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani "kwa maneno makali" shambulio la Hamas dhidi ya miji ya Israel, Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric ameeleza leo Jumamosi.

"Mashambulizi hayo hadi sasa yamegharimu maisha ya raia wengi wa Israel na kujeruhi mamia," Bwana Dujarric amesema na kuongeza "Katibu Mkuu ameshangazwa na ripoti kwamba raia wamevamiwa na kutekwa nyara kutoka kwa nyumba zao."

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa anaguswa sana na raia na anatoa wito wa kujizuia zaidi na kwamba "juhudi zote za kidiplomasia" zinafanywa "kuepusha moto mkubwa zaidi", Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema. "Raia lazima waheshimiwe na kulindwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu wakati wote."

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa watu wote waliotekwa nyara.

"Anasisitiza kwamba ghasia haziwezi kutoa suluhu kwa mzozo huo, na kwamba ni kwa njia ya mazungumzo tu ya kuleta suluhu ya Serikali mbili ndipo amani inaweza kupatikana," Msemaji wa Umoja wa Mataifa ameeleza.

Mratibu Maalum wa UN

"Haya ni mashambulizi ya kuchukiza kwa raia ambayo lazima yakome mara moja," amesema Tor Wennesland ambaye ni Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati wakati akilaani vikali shambulio la wanamgambo wa Hamas dhidi ya majiji na miji ya Israel karibu na ukanda wa Gaza lililotekelezwa leo asubuhi ya Jumamosi saa za Israel. 

Kupitia taarifa aliyoitoa Wennesland akiwa Jerusalem – Israel, amesema, matukio haya, yamesababisha matukio ya kutisha ya vurugu na vifo vingi na majeraha kwa Waisraeli, ambao wengi wao wanaaminika kutekwa nyara na kupelekwa Ukanda wa Gaza. 

Bwana Wennesland amesema ana mawasiliano ya karibu na pande zote zinazohusika na kuwataka watumie wajizuie na pia walinde raia. 

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa naye ashitushwa 

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk "ameshtushwa na kufadhaishwa na ripoti kwamba mamia, na pengine maelfu, ya makombora ya kiholela yamerushwa na makundi yenye silaha ya Palestina huko Israel, na kwamba Waisraeli wasiopungua 22 wameuawa na mamia kujeruhiwa." 

"Pia nina wasiwasi mkubwa na ripoti kwamba raia wa Israeli wamechukuliwa mateka," Turk ameongeza. "Shambulio hili lina athari ya kutisha kwa raia wa Israeli." Amebainisha kuwa raia haipaswi kwa hali yoyote kuwa walengwa wa mashambulizi. 

Taarifa hiyo ya Turk iliyosambazwa Jumamosi hii kutoka Geneva, Uswisi pia imebainisha kuwa wanajeshi wa Israel walijibu mashambulizi ya anga kwenye Ukanda wa Gaza wenye wakazi wengi, ambayo yanaripotiwa kuwaua takriban watu watano.  

Volker Türk ametoa wito kwa vikosi vya usalama vya Israel kuchukua tahadhari zote ili kuepusha maafa ya raia. 

"Ninatoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa ghasia na kutoa wito kwa pande zote na nchi muhimu katika kanda kupunguza kasi ili kuepusha umwagaji damu zaidi," Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza. 

Rais wa Baraza Kuu

Tweet URL

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Dennis Francis ameandika katika mtandao wa kijamii wa X akilaani vikali “shambulio la wanamgambo wa Hamas dhidi ya Israel, ambalo limeua na kujeruhi mamia ya raia wasio na hatia.” 

“Pole zangu za dhati kwa familia na jamaa wa waathirika. Ninatoa wito kwa pande zote kujiepusha na vurugu zaidi na kutafuta njia ya haraka ya amani.” 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitangaza kuwa litafanya mkutano wa faragha Jumapili mchana kujadili suala hilo Pamoja na mambo mengi.