Huduma za afya kwa wakimbizi zaimarika, ukosefu wa damu bado tishio- Ripoti

20 Julai 2018

Ripoti mpya ya shirika la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR kuhusu afya ya wakimbizi imebaini kuwa huduma za afya kwa kundi hilo pamoja na wengine waliofurushwa makwao ziko kwenye mwelekeo sahihi licha ya kwamba ukosefu wa damu, kudumaa na magonjwa ya kuambukiza bado ni tishio.

Ikipatiwa jina la mtazamo wa kila mwaka wa afya ya umma kwa dharura mpya za wakimbizi, ripoti inataja sababu ya mafanikio hayo kuwa ni ufuatiliaji wa kila mwaka wa vigezo muhimu vya afya kwa wakimbizi wakati wa dharura, hatua ambayo imewezesha kuchukua hatua haraka pindi dharura inapotokea.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa UNHCR Andrej Mahecic ametaja vidokezo vinavyofuatiliwa kuwa ni afya ya uzazi, Ukimwi, lishe, uhakika wa chakula na maji safi na huduma za kujisafi katika operesheni muhimu 37 za kuhudumia wakimbizi.

Amesema operesheni 21 kati ya hizo, UNHCR na wadau wake hukusanya na kuchambua takwimu kwa kutumia vigezo kwenye mfumo wa pamoja ili kulinda na kuhudumia vizuri wakimbizi.

Mathalani kwenye upande wa vifo miongoni mwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano, ripoti inasema licha ya  kuwepo kwa idadi kubwa ya wakimbizi mwaka 2017, bado wastani wa vifo ulikuwa 0.4 kwa mwezi kwa kila watoto 1000 wakimbizi.

Bwana Mahecic amesema kiwango hicho kimo ndani ya kiwango cha vifo kwa  nchi zinazoendelea na zile za kipato cha kati, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu vifo ya mwaka 2017.

Mtoto mkimbizi wa Rohingya anapatiwa chanjo ya polio katika kituo cha chanjo cha Bormapara, eneo la Cox's Bazar, Bangladesh.
UNICEF/Bashir Ahmed Sujan
Mtoto mkimbizi wa Rohingya anapatiwa chanjo ya polio katika kituo cha chanjo cha Bormapara, eneo la Cox's Bazar, Bangladesh.

 

Kuhusu afya ya uzazi amesema, “kumekuwepo na maendeleo kwenye huduma za afya ya  uzazi kwa kuwa wajawazito 9 kati ya 10 walijifungua chini ya  usimamizi wa mhudumu wa afya mwenye ujuzi. Kiwango hicho ni ongeeko la asilimia 25 ikilinganishwa na mwaka 2016.”

Zaidi ya yote amesema takribani wajawazito 500,000 walipata huduma kabla ya kujifungua katika vituo 135 ambavyo vinafuatilia kwenye operesheni hizo 21, kiwango ambacho ni ongezeko kwa asilimia 18 ikilinganishwa na mwaka jana.

Viwango vya kudumaa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa 25% vimebaki kama 2016

Hata hivyo amesema licha ya mafanikio hayo bado wana wasiwasi mkubwa juu ya ongezeko la idadi ya wakimbizi wenye ukosefu wa damu na wanaodumaa kutokana na ukosefu wa lishe bora.

“Viwango vya kudumaa miongoni mwa watoto wenye  umri wa chini ya miaka mitano kwenye asilimia 25 ya operesheni zetu vimesalia kama ilivyokuwa mwaka 2016. Zaidi ya asilimia 50 ya maeneo yaliyokaguliwa, kuna kiwango cha juu sana cha ukosefu wa damu miongoni mwa watoto,” amesema Mahecic.

Ni kwa mantiki hiyo amerejelea wito wa UNHCR kupatiwa fedha ambazo wameomba kwa mwaka huu wa 2018 ili kuweza kukidhi mahitaji ya kiafya ya wakimbizi akisema kati ya dola bilioni 8.275 walizoomba, hadi sasa wamepokea asilimia 33 pekee.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter